• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Bakken Bears anayochezea Tylor Ongwae yapigwa breki baada ya ushindi 18 mfululizo Denmark

Bakken Bears anayochezea Tylor Ongwae yapigwa breki baada ya ushindi 18 mfululizo Denmark

Na GEOFFREY ANENE

REKODI ya kushinda michuano 18 mfululizo kwenye Ligi Kuu ya Mpira wa vikapu ya Denmark ya Bakken Bears anayochezea Mkenya Tylor Ongwae Okari ilivunjiliwa mbali na Svendborg Rabbits baada ya kupigwa 103-97 uwanjani Rise Sparekasse Arena, Jumatano.

Bears, ambayo ilikuwa inafukuzia ushindi wa 20 mfululizo katika mashindano yote, ilianza mechi hiyo vibaya ilipopoteza robo ya kwanza kwa alama 27-21.

Vijana wa Steffen Wich, ambaye alikuwa anakaribisha nyota wake wa kimataifa akiwemo Ongwae aliyeongoza Kenya kutinga Kombe la Afrika (AfroBasket) mwezi uliopita kwa mara ya kwanza tangu 1993, walishinda robo ya pili pembamba 22-21.

Walipoteza mwelekeo tena katika robo ya tatu 32-17 na, ingawa walijikakamua na kutwaa robo ya mwisho 37-23, hawakuwa wamefanya ya kutosha kudumisha rekodi yao iliyoanza ligini mnamo Oktoba 16, 2020 walipokung’uta Amager 128-59 na katika mashindano yote mnamo Novemba 20, 2020 walipobwaga Bears Academy 92-80.

Hapo Jumatano, wachezaji watatu wa kwanza katika ufungaji wa alama walitoka Bears. Wachezaji hao ni Ryan Evans na Deshawn Stephens (20 kila mmoja) na QJ Peterson (17). Brandon Norfleet alifungia Rabbits alama nyingi (16). Ongwae alichangia alama tano pekee katika dakika 19 alizochezeshwa.

Kichapo hicho kilikuwa cha kwanza cha Bears mikononi mwa Rabbits katika mechi 23. Mara ya mwisho Bears ilikuwa imepoteza dhidi ya wapinzani hao ni Desemba 7 mwaka 2015 ilipolazwa 102-98 katika muda wa ziada baada ya muda wa kawaida kutamatika 93-93.

Bears, ambayo inatafuta kushinda ligi hiyo kwa msimu wa tano mfululizo, itakutana na Team FOG Naestved katika mechi yake ijayo mnamo Machi 12.

  • Tags

You can share this post!

Kampeni chanjo ya corona ipewe wanamichezo wa Kenya...

Were aongoza Zesco United kutesa ligini Zambia NAPSA Stars...