• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:02 AM
Balaa belua wazee 3 wakiuawa kwa madai ya ushirikina

Balaa belua wazee 3 wakiuawa kwa madai ya ushirikina

Na SIAGO CECE

HOFU imetanda katika Kaunti ya Kwale baada ya visa vya mauaji ya wazee kuchipuka upya.

Katika miaka iliyopita, Kaunti ya Kwale na Kilifi zilishuhudia aina nyingi ya visa aina hii ambapo wazee waliuawa kwa madai ya kuwa wachawi, lakini vikapungua kwa kiasi kikubwa hasa maeneo ya Kwale kufuatia ushirikiana kati ya juhudi za idara ya usalama na jamii.

Hata hivyo, mauaji ya wazee watatu katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita yamelazimu idara ya polisi kuweka mikakati upya.Mauaji hayo yamefikisha idadi ya wazee waliouawa mwaka huu pekee kufika 12.

Kamishna wa Kaunti ya Kwale, Bw Joseph Kanyiri alisema kwamba visa hivyo vinavyotokana na mzozo wa urithi wa mali ya familia vimekithiri katika maeneo ya Lungalunga na Kinango.

Akizungumza katika afisi yake mjini Kwale, Bw Kanyiri alisema maafisa wa polisi wanaendeleza upelelezi kuvihusu.

“Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa wazee waliolengwa wana umri wa zaidi ya miaka 70, na wanazo mvi vichwani mwao. Pia imebainika mauaji yanatendwa na jamaa zao ambao wanashutumu wazee hawa kuwa wachawi,” akasema.

Kisa cha majuzi zaidi kilikuwa cha mwanamke mwenye umri wa miaka 90 ambaye aliuawa, akachomwa na mwili wake kufichwa katika eneobunge la Lungalunga hivi majuzi.

Kulingana na Bw Kanyiri, washukiwa wakuu ni jamaa za ajuza huyo kwani hakuna hata mmoja wao aliripoti kisa hicho hadi mwili wa mwanamke ulipopatikana na majirani.

Kamishna huyo alisema kuwa tayari polisi wanafuatilia kesi hiyo ili kuona kwamba washukiwa wanakamatwa na kushtakiwa.

Wenyeji wa Kwale waliohojiwa na Taifa Leo walisema kuwa katika visa vingi, jamaa wa waathiriwa hasa vijana ndio huhusika.

Imedaiwa kuwa wao hulipa magenge kutekeleza mauaji aina hiyo kwa kisingizio cha ushirikina, ilhali wanataka wapate nafasi ya kurithi ardhi na mali nyingine zinazoachwa na marehemu.

“Vijana wengi wanataka mali za haraka. Hakuna ajira wanazoweza kutegemea na wengine wao ni wazembe kujitafutia riziki kivyao kwa hivyo wanataka njia za mkato kurithi mali, lakini mauaji hayastahili kamwe,” akasema mkazi aliyeomba kutotajwa jina kwa kuhofia kuwa kufanya hivyo kutahatarisha maisha yake.

Matukio haya yamesababisha baadhi ya wazee walio na nywele zenye mvi kuhama makwao kwa sababu za kiusalama wakihofia kutuhumiwa kuwa wachawi.

You can share this post!

Wafanyakazi 9 wafa kwa kuanguka na kreni

Cristiano Ronaldo arejea Manchester United baada ya kuagana...