• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
Cristiano Ronaldo arejea Manchester United baada ya kuagana na Juventus ya Italia

Cristiano Ronaldo arejea Manchester United baada ya kuagana na Juventus ya Italia

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wamethibitisha kwamba wameafikiana na Juventus kuhusu mpango wa kumsajili upya fowadi matata raia wa Ureno, Cristiano Ronaldo kwa mkataba wa miaka miwili.

Man-United wamefanikisha usajili huo wa Ronaldo, 36, kwa kima cha Sh1.9 bilioni kabla ya kujumuishwa kwa mahitaji mengine ya kibinafsi, visa ya usafiri na gharama za matibabu.

Katika msimu wake wa kwanza uwanjani Old Trafford, Ronaldo alifungia Man-United jumla ya mabao 118 kutokana na mechi 292 kabla ya kuondoka na kuyoyomea Uhispania mnamo 2009 kuvalia jezi za Real Madrid.

Juventus waliweka mezani kima cha Sh15.4 bilioni mnamo Julai 2018 ili kumshawishi Ronaldo kuagana na Real Madrid ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

“Kila mmoja ana hamu ya kumkaribisha tena Ronaldo uwanjani Old Trafford,” ikasema sehemu ya taarifa fupi ya Man-United.

Tangazo la kusajili kwa Ronaldo kambini mwa Man-United lilipata mashabiki wengi kwa mshangao ikizingatiwa kwamba sogora huyo alikuwa akihusishwa pakubwa na Manchester City.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City wamekuwa wakitafuta fowadi wa kujaza pengo la Sergio Aguero aliyetua Barcelona. Juhudi zao za kumsajili Harry Kane wa Tottenham Hotspur ziliambulia pakavu.

Akiwa Man-United ambao walijivunia huduma zake kwa kipindi cha miaka sita, Ronaldo alitwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), mawili ya League Cup na ufalme wa Kombe la FA. Aidha, alinyanyua Kombe la Dunia na Community Shield chini ya kocha mstaafu Sir Alex Ferguson.

Akizungumza na wanahabari mnamo Ijumaa baada ya kuongoza Man-City kujiandaa kwa mechi ya EPL dhidi ya Arsenal, Guardiola alisema: “Ronaldo ni mchezaji wa Juventus ingawa lolote linaweza kufanyika katika kipindi kifupi kijacho.”

“Wapo wachezaji wachache sana, akiwemo Ronaldo na Lionel Messi, ambao wana uwezo wa kuamua wanakotaka kuchezea,” akaongeza Guardiola.

Kwa mujibu wa kocha Ole Gunnar Solskjaer, miongoni mwa watu waliochangia pakubwa kumshawishi Ronaldo kurejea Man-United badala ya kujiunga na Man-City ni kiungo raia wa Ureno, Bruno Fernandes.

Ronaldo anakuwa mchezaji wa tatu wa haiba kubwa kujiunga na Man-United muhula huu baada ya Jadon Sancho na Raphael Varane waliotokea Borussia Dortmund na Real Madrid mtawalia.

ITHIBATI RONALDO NI MIONGONI MWA WANASOKA BORA ZAIDI DUNIANI:

  • Mshindi mara tano wa Ballon d’Or mnamo 2008 (akiwa Man-United) na 2013, 2014, 2016 na 2017 (akiwa Real Madrid).
  • Mshindi mara tano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2008 (akiwa Man-United) na 2014, 2016, 2017 and 2018 (akiwa Real Madrid).
  • Mshindi mara saba wa mataji ya Ligi Kuu akishiriki ligi tatu tofauti mnamo 2007, 2008, 2009 (akiwa Man-United), 2012 na 2017 (akiwa Real Madrid), 2019, 2020 (akiwa Juventus).
  • Mshindi wa Euro mnamo 2016 akivalia jezi za Euro
  • Mshindi wa mataji 32 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa akivalia jezi za Sporting Lisbon, Manchester United, Real Madrid, Juventus na Ureno
  • Mfungaji bora wa muda wote katika kampeni za UEFA (mabao 134 kutokana na mechi 176).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Balaa belua wazee 3 wakiuawa kwa madai ya ushirikina

Vita vya kujipima nguvu ugavana Kiambu vyaanza