• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Wafanyakazi 9 wafa kwa kuanguka na kreni

Wafanyakazi 9 wafa kwa kuanguka na kreni

Na COLLINS OMULO

WATU tisa Alhamisi walikufa na wengine kujeruhiwa baada ya kreni waliokuwa ndani yake eneo la ujenzi kuanguka.

Miongoni mwa waliokufa ni Wakenya saba na raia wawili wa China waliokuwa kwenye kreni hiyo katika eneo la ujenzi mtaani Hurlingham jijini Nairobi.

Polisi wa eneo la Kilimani, Andrew Mbogo, alithibitisha tukio hilo akisema kuwa kreni hiyo ilianguka mwendo wa saa sita unusu wakati waathiriwa hao 10 walikuwa wakiitengeneza.

“Wafanyakazi 10 walikuwa ndani ya kreni hiyo. Tisa walikufa papo hapo na mmoja akapata majeraha,” akasema Bw Mbogo.

Alisema kuwa mfanyakazi mmoja aliyejeruhiwa alikimbizwa katika Hospitali ya Nairobi Women na miili ya waliokufa kuhifadhiwa katika mochari ya Chiromo.

Hata hivyo, Bw Mbogo alieleza kuwa uchunguzi umeanzishwa ili kutathmini kilichosababisha kreni hiyo kuanguka.

“Tulifikiri kuwa huenda wengine waligongwa pia na kreni hiyo katika eneo hilo la ujenzi ila msimamizi wa ujenzi huo alisema wafanyakazi wengine walikuwa salama,” akaongeza Bw Mbogo.

Kulingana na mmoja wa wafanyakazi hao, Michael Odhiambo, tukio hilo liliwashtua na hata kuwafanya wakimbilie usalama.

“Tuliporudi kuangalia kilichoanguka kwa kishindo, tulikuta kuwa ni kreni. Miili ya waliokuwa kwenye kreni ilikuwa chini,” akasema Bw Odhiambo.

Alisema kuwa wanaoshughulika na kreni hiyo ni wajenzi wanaofahamika katika eneo hilo.

“Ni mmoja tu aliyenusurika kwa sababu alifunga mshipi. Wengine tisa walirushwa kutoka kimo cha mita sabini,” akaongeze Bw Odhiambo.

Ujenzi huo uliosimamiwa na wahandisi wa nchi ya China ZICC ulikuwa chumba cha wanafunzi.

Meneja mkuu wa ZICC Kenya, Zong Xudong, alisema kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi ili kutathmini kilichosababisha kreni hiyo kuanguka.

“Tayari timu yetu inayosimamia ajali za dharura imeanza mchakato wa kufikia familia za waathiriwa,” akasema Bw Xudong.

You can share this post!

Raila: Sehemu muhimu za chanjo ni sokoni, shuleni

Balaa belua wazee 3 wakiuawa kwa madai ya ushirikina