• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Bei ya stima itapanda mpende msipende, mshauri wa Ruto aambia Wakenya

Bei ya stima itapanda mpende msipende, mshauri wa Ruto aambia Wakenya

Na LEONARD ONYANGO

MATUMAINI ya Wakenya kupata umeme nafuu huenda yakadidimia baada ya serikali ya Kenya Kwanza kushikilia kuwa haina mpango wa kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu.

Mwenyekiti wa Baraza la Kushauri Rais kuhusu Uchumi, Dkt David Ndii, jana alisema kuwa Rais William Ruto hakuahidi kupunguza bei ya umeme katika manifesto yake.

Dkt Ndii aliwataka raia kujiandaa kwa ajili ya mambo mawili; kutumia umeme ghali usiokatika mara kwa mara au umeme nafuu unaokatika kila mara.

Alidai kuwa nchini Afrika Kusini wanatumia umeme nafuu unaopotea kwa saa kadhaa kila siku.

“Katika manifesto ya Kenya Kwanza hatukuahidi kuwa tutawapa umeme wa bei nafuu,” akasema Dkt Ndii.

Mshauri huyo wa Rais Ruto alitoa kauli hiyo huku kampuni ya kusambaza umeme nchini, Kenya Power, ikipendekeza kupandishwa kwa bei ya stima kuanzia Aprili, mwaka huu.

Bei ya juu ya umeme na mafuta ndicho kiini cha kupanda kwa gharama ya maisha nchini.

Rais Ruto, kupitia manifesto ya Kenya Kwanza, anakiri kuwa umeme ghali unatatiza uchumi na huduma kama vile afya, usalama na ubora wa maisha.

Rais Ruto pia anasema kuwa sababu kuu ya umeme kukatika mara kwa mara nchini ni matumizi ya nyaya na mitambo kuukuu.

“Kenya ina utajiri wa kawi ya mvuke, jua, upepo na maji. Tunaweza kupata umeme nafuu kutokana na vyanzo hivi,” anasema.

“Tunapendekeza mambo matatu yanayoweza kusaidia kupunguza gharama ya umeme nchini: kukarabati mtandao wa kusambaza umeme, kuongeza kasi ya uzalishaji wa kawi ya mvuke, kuendeleza kituo cha kuhifadhi gesi jijini Mombasa.”

  • Tags

You can share this post!

Mchecheto NATO ikituhumu China kusaidia Urusi kuipiga...

TAHARIRI: Ni aibu Ukraine kuipa Kenya msaada wa mlo

T L