• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
BENSON MATHEKA: TSC iwe na uwazi na usawa katika mpango wa mafunzo

BENSON MATHEKA: TSC iwe na uwazi na usawa katika mpango wa mafunzo

Na BENSON MATHEKA

Mafunzo ambayo Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) imeagiza walimu kuanza ili kukuza taaluma yao yamegubikwa na usiri na utata mkubwa ambao unaweza kuathiri taaluma hiyo na sekta ya elimu kwa jumla.

Ingawa kila sekta huwa na mpango wa kukuza wataalamu wake kupitia mafunzo kuhusiana na masuala ibuka, unapaswa kuwa na uwazi, mashauriano na uadilifu katika hatua hiyo.

Taaluma kama uanasheria, udaktari na uhandisi zina mpango wa mafunzo endelevu kwa wanachama wake ambao hufanyika kwa uwazi. Mafunzo hayo hufanikishwa na vyama au mashirika ya kudhibiti taaluma hizo na huwa ni ya lazima kwa wanachama chini ya taratibu zilizokubaliwa.

Inashangaza basi, mpango wa kuwapa walimu mafunzo unabuniwa na mwajiri wao ambaye amewapa masharti makali kutimiza bila kushauriana na walimu moja kwa moja au kupitia vyama vinavyowawakilisha.

Japo TSC inaweza kuwa na nia nzuri kwa kuanzisha mpango huo, kuteua vyuo vikuu vitatu pekee miongoni mwa 20 vilivyoidhinishwa ni kuonyesha ukosefu wa usawa na uwazi.

Kulingana na tume hiyo, ni vyuo vikuu vya Riara, Mt Kenya na Kenyatta vilivyoteuliwa kutoa mafunzo yatakayogharimu walimu zaidi ya Sh2 bilioni kwa mwaka.

Riara na Mt Kenya ni vyuo vikuu vya kibinafsi na inashangaza kwa nini vile vya umma vilivyo maeneo tofauti nchini viliachwa nje ya mpango huo.

Kuna kesi kortini kuhusu suala hili na TSC inafaa kufafanua zaidi kuhusu mpango huo ili isionekane kuhujumu na kuwanyanyasa walimu wakati ambao wanahitajika kuwa shuleni kutekeleza mtaala mpya wa elimu.

Kinachoashiria kuwa mpango huo haukufanywa kwa uwazi ni kukashifiwa na wabunge ambao wanapaswa kupiga darubini utendakazi wa idara na mashirika ya serikali.

TSC inafaa kuchunguza upya mpango huo isionekane kuwa inaendeleza juhudi za kudhulumu walimu ilizoanza kwa kulenga vyama vinavyotetea maslahi yao.

Tume hiyo imelaumiwa mara sio moja kwa kuhujumu na kugawanya viongozi wa vyama vya wafanyakazi, kuhamisha walimu kutoka kaunti wanazotoka na kuweka kandarasi za utendakazi ambazo walimu hutia saini kila mwaka hasa walimu wakuu.

Ili kuleta uwazi katika mpango huo ambao kwa kweli sio mbaya, tume inafaa kuruhusu vyuo vikuu vyote vinavyotoa mafunzo ya ualimu kuyafanikisha.

Hii itapunguzia gharama walimu ambao watalazimika kusafiri hadi kuliko matawi ya vyuo vikuu vitatu vilivyoteuliwa. Itakuwa muhimu pia iwapo tume itaita mkutano wa wadau kueleza mbinu iliyotumia kuteua vyuo hivyo vitatu.

You can share this post!

Tumejifunza kutokana na makosa yetu ya zamani , KANU Fresh...

CHARLES WASONGA: SGR kuelekea Malaba itapiga jeki biashara