• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
CHARLES WASONGA: SGR kuelekea Malaba itapiga jeki biashara

CHARLES WASONGA: SGR kuelekea Malaba itapiga jeki biashara

Na CHARLES WASONGA

TANGAZO la Shirika la Reli nchini (KRC) kwamba huduma za treni kati ya Mombasa na miji ya Kisumu na Malaba zitaaza tena Novemba mwaka huu ni habari njema kwa wafanyabiashara wa humu nchini.

Vilevile, kurejeshwa kwa huduma hizo za uchukuzi wa bidhaa na abiria kutachochea ukuaji wa uchumi ambao umeathiriwa pakubwa na makali ya Covid-19, miongoni mwa changamoto nyinginezo.

Mkurugenzi Mtendaji wa KRC, Philip Mainga wiki jana alisema kuwa huduma hiyo itafanikishwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa reli inayounganisha reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Mai Mahiu na reli ya zamani katika eneo la Longonot karibu na mji wa Naivasha.

Afisa huyo aliambia wabunge wanachama wa Kamati ya Fedha kwamba ujenzi wa reli hiyo mpya uligharimu Sh3.5 bilioni.

Mradi wa ukarabati wa reli ya zamani kutoka Naivasha hadi mji wa Malaba ulioko katika mpaka wa Kenya na Uganda na laini ya kutoka Nakuru hadi Kisumu uligharimu jumla ya Sh3.8 bilioni.

Kwa hivyo, kwa kutumia Sh7.3 bilioni pekee, shirika la KRC litawezesha uchukuzi wa bidhaa na abiria kutoka Mombasa hadi taifa jirani la Uganda, kupitia mji wa Malaba, kwa gharama nafuu.

Aidha, mizigo kutoka Mombasa itasafirishwa hadi Kisumu kisha ipakiwe kwa meli katika bandari mpya ya Kisumu na kusafirishwa hadi Uganda.

Ukarabati wa bandari hiyo uligharimu Sh3.2 bilioni.Hii itaimarisha biashara kati ya Kenya na mataifa jirani ya Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda ambayo hayajapakana na bahari.

Kwa mfano, kulingana na takwimu za hivi punde zilizotolewa na Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) Kenya iliuza bidhaa za Sh24.04 bilioni kati ya Mei na Juni mwaka huu.

Hii ni mbali na mapato kutoka kwa bidhaa zilizouzwa Uganda, ikiwemo mafuta, ambayo hutua katika bandari ya Mombasa na kusafirishwa kwa barabara hadi Uganda.

Hivi majuzi, Rais wa DRC, Felix Tshisekedi alizuru nchini na kutia saini mkataba wa kibiashara wa thamani ya Sh92 bilioni kwa mwaka kati ya nchi yake na Kenya.

Kwa hivyo, sasa ni wajibu wa Kenya kupalilia uhusiano mzuri wa kidiplomasia na mataifa haya jirani ili iweze kufaidika kibiashara.

Kunawiri kwa biashara kati ya Kenya na mataifa haya bila shaka kutaliletea taifa hili mapato yatakayoliwezesha kupunguza zigo la madeni linayodaiwa na mataifa ya nje hasa China.

Kufufuliwa kwa shughuli za uchukuzi kwa reli kati ya Mombasa na miji ya Kisumu na Malaba pia kutawezesha mradi wa SGR kuvuna faida kubwa, hususan, kupitia usafiirishaji wa mizigo hadi maeneo ya bara na mataifa jirani.

Tangu kuzinduliwa kwa huduma za uchukuzi wa bidhaa kupitia reli hiyo mpya, mapato kutokana na uchukuzi wa mizigo imekuwa finyu zaidi hali iliyotilia shaka faida ya mradi huo wa SGR uliogharimu Sh347 bilioni.Aidha, laini kutoka Nairobi hadi Mai Mahiu iligharimu Sh150 bilioni, pesa ambazo zilikopwa kutoka serikali ya China.I

sitoshe, kurejelewa kwa safari za treni kutoka Nakuru hadi Kisumu na hatimaye Butere kutaimarisha biashara katika miji ya Molo, Elburgon, Londiani, Koru, Muhoroni na Chemelil ambayo ilififia baada ya kusitishwa kwa huduma hizo miaka 15 iliyopita.Changamoto sasa ni kwa serikali na shirika la KRC kuhakikisha inatoa huduma bora na za kutegemewa na wateja.

You can share this post!

BENSON MATHEKA: TSC iwe na uwazi na usawa katika mpango wa...

Mkenya azuiliwa Uhispania kwa kugeuka mla watu