• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Bodaboda, wanachuo wapanda migomba kwenye barabara mbovu wakilalamikia tope kila mahali

Bodaboda, wanachuo wapanda migomba kwenye barabara mbovu wakilalamikia tope kila mahali

NA WYCLIFFE NYABERI

Waendeshaji pikipiki na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kisii Jumatatu Novemba 6, 2023 walipanda migomba kwenye barabara ya Nyakomisaro-Bobaracho kulalamikia hali yake mbaya huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha nchini.

Wakazi hao waliojawa na ghadhabu walisema barabara hiyo imekuwa ngumu kupitika na juhudi zao za kuwafikia viongozi wa eneo hilo ili kupata suluhu zimeambulia patupu. Hivyo basi, waliamua kuchukua uamuzi wa kuziba barabara hiyo kwa kupanda migomba ya ndizi kwenye barabara hiyo.

Yvonne Moraa, mama mwenye nyumba za kukodisha eneo la Nyamage, alisema wanafunzi wa chuo kikuu walikuwa wameanza kuhama nyumba zao kwa sababu ya tope jingi linalowakera.

“Kuna matope kote. Wanachuo wanahama maeneo haya kwa sababu hawataki kuingia masomoni wakiwa wamechafuka. Wanaepuka eneo hili kama ndwele na tunakodolea hasara tele,” Bi Moraa alisema.

Maoni yake yaliungwa mkono na Bw Zablon Ondieki aliyesema tangu 2017, wamekuwa wakimtafuta diwani wa eneo hilo kuomba usaidizi wa kuboresha barabara hiyo lakini hakuna suluhu yoyote iliyopatikana.

“Vilio vyetu havisikiwi na yeyote. Leo, tumeamua kuchukua hatua hii kushinikiza barabara hiyo irekebishwe kwani tumechoka,” Bw Ondieki alisema.

Aliongeza kuwa viongozi wa eneo hilo wamekuwa wakiwashirikisha katika michezo ya paka na panya juu ya ni nani aliye na jukumu la kukarabati barabara hiyo.

“Kila tukifika afisi ya MCA, tunaambiwa barabara si yake. Pia tunasimuliwa habari hizo hizo tukitua kwa Mbunge. Viongozi wote waliochaguliwa wanapokataa jukumu la kutengeneza barabara, tunashangaa kinachoendelea,” Bw Ondieki aliongeza.

Tunatoa wito kwa Gavana Simba Arati kuingilia kati suala hilo. Inasikitisha kuwa tunaweza kuwa na barabara kama hizi katika karne ya 21 karibu na taasisi za elimu,” Enoch Matoke, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Kisii alilalamika.

  • Tags

You can share this post!

Mashabiki wa Shabana waweka historia kwa kujaza uwanja wa...

Majambazi wavamia makazi ya MCA Kisii usiku kukinyesha,...

T L