• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Majambazi wavamia makazi ya MCA Kisii usiku kukinyesha, waponyoka na simu za Sh60,000

Majambazi wavamia makazi ya MCA Kisii usiku kukinyesha, waponyoka na simu za Sh60,000

NA WYCLIFFE NYABERI

Polisi mjini Kisii wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo majambazi walivamia nyumba ya diwani wa Bobaracho Ibrahim Ongubo Mose Jumapili usiku.

Genge la majambazi wanane waliingia katika jumba la kifahari la Bw Ongubo katika kijiji cha Nyataro, dakika chache baada ya saa mbili za usiku. Diwani huyo alikuwa akila chajio na familia yake walipovamiwa.

Majambazi hao wanaosemekana kujihami na bunduki na silaha zingine butu, walitaka kujua diwani huyo alikuwa kwenye chumba kipi kutoka kwa wale waliokutana nao kwanza.

Wahalifu hao waliruka ndani ya boma la Bw Ongubo kutoka sehemu ya nyuma ya nyumba yake muda mfupi baada ya yeye kuwasili nyumbani.

“Ilikuwa dakika chache baada ya saa mbili. Nilikuwa nimetoka kumfungulia lango. Kwa vile mvua ilikuwa inanyesha, nilikwenda jikoni kuota moto. Nilikuwa nishafika watu wawili waliponifuata na kuanza kuniuliza Mheshimiwa yuko wapi,” Joseph Mong’are, mlinzi katika makazi ya Bw Ongubo alisema.

Akihutubia wanahabari baada ya shambulio hilo, Bw Ongubo alikashifu kisa hicho.

“Utovu wa usalama umeanza kutanda Kisii. Visa hivi vilikuwepo miaka iliyopita lakini maafisa wa polisi kwa ushirikiano na Nyumba Kumi walikomesha uhalifu huo na wakazi wengi walifurahia. Inasikitisha kwamba visa hivyo tena vinarejea kwa kasi,” Bw Ongubo alisema.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kisii ya Kati Isaac Kimwele alipuuza habari kwamba majambazi hao walikuwa na bunduki.

“Watu walisema kuwa walifyatua risasi hewani mara tatu lakini hizo hazikuwa risasi za bunduki. Walitumia njia nyingine za kuwatisha watu na tunawaomba umma kuwa watulivu kwani tumeanzisha uchunguzi,” Bw Kimwele aliambia Taifa Leo kwa simu.

  • Tags

You can share this post!

Bodaboda, wanachuo wapanda migomba kwenye barabara mbovu...

Wanaume hawawezi kustahimili habari mbaya kama wanawake...

T L