• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
CBC: Magoha apuuza malalamishi ya wazazi

CBC: Magoha apuuza malalamishi ya wazazi

Na WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, jana alipuuza vikali malalamishi ambayo yamekuwa yakitolewa na wazazi kuhusu gharama ya juu ya Mfumo wa Elimu ya Umilisi na Utendaji (CBC), akishikilia hatarejea nyuma.

Wazazi wamekuwa wakilalamika vikali kuhusu gharama ya juu ya mfumo huo, baadhi wakisema wanashindwa kununua baadhi ya vifaa wanavyohitajika kuwanunulia wanao kama vitabu.

Hata hivyo, Prof Magoha alipuuzilia mbali malalamishi hayo, akiyataja kutolewa na watu “ambao hawajaelimika.”

“Wanaolalamika kuhusu gharama ya juu ya mfumo huu wanapuuza uhalisia uliopo. Ni watu ambao hawakuenda shuleni. Hatutarejea nyuma kwenye juhudi za utekelezaji wa mfumo huu,” akasema Prof Magoha, huku akiusifia kuwa “njia bora zaidi ya kuleta mageuzi kamili katika sekta ya elimu nchini.”

Kando na gharama ya vitabu, wazazi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa mwongozo na utaratibu maalum kutoka kwa Wizara ya Elimu kuhusu namna wanavyopaswa kuwasaidia wanao kufanya kazi za ziada wanazopewa na walimu wao.

Wadau katika sekta hiyo vile vile wamekuwa wakilalamika kuhusu ukosefu wa baadhi ya vifaa wanavyohitajika kuwa navyo ili kufanya mazoezi wanayopewa.

Katika kile kilionekana kama hatua ya serikali kuanza kushughulikia baadhi ya malalamishi hayo, waziri aliwahimiza walimu na wasimamizi wakuu wa elimu katika kiwango cha kaunti ndogo kuanza vikao kuwapa ufafanuzi wazazi kuhusu yale wanayohitajika kufahamu kuhusu mfumo huo.

“Lazima wadau wote katika sekta hii kuungana ili kusuluhisha baadhi ya masuala yanayoendelea kuibuka,” akaeleza.

Wakati huo huo, serikali jana ilitangaza kuwa kufikia sasa, walimu 229,000 wamepata mafunzo maalum kuhusu mfumo huo.

Kulingana na Katibu wa Idara ya Utekelezaji wa Mfumo wa CBC, Prof Fatuma Chege, utaratibu huo utaendelea hadi pale walimu katika viwango vyote watapokea mafunzo hayo.

“Utekelezaji wa mfumo huu ni jambo litakaloendelea kwa hatua. Tutaendelea kutoa mafunzo kwa hatua kwa kila mwalimu,” akasema Prof Chege.

Kikao hicho kilikuwa kimeandaliwa na Baraza la Wahariri Kenya (KEG) katika hoteli moja jijini Nairobi kutathmini hatua zilizofikiwa kwenye utekelezaji wa mfumo huo.

You can share this post!

Historia bei ya petroli ikigonga Sh134

Shughuli kama nyuki JKIA wanariadha wakianza kumiminika kwa...