• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:50 AM
Covid: Raia lawamani kwa kupuuza kanuni

Covid: Raia lawamani kwa kupuuza kanuni

STANLEY KIMUGE na O. K’ONYANGO

HATUA za kujitibu, itikadi za kitamaduni na kusongamana katika maeneo ya umma kama vile vilabu, benki na maduka ya jumla zimehusishwa na kuongezeka kwa visa vya Covid-19 katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Kaunti hiyo imezidiwa na maambukizi ya Covid-19 huku vituo vingi vya afya vikikabiliwa na ukosefu wa vitanda katika Vitengo vya Wagonjwa Mahututi (ICU).

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo unaashiria kuwa wakazi wengi wamepuuzilia mbali masharti baadhi wakikosa kuvalia barakoa hadharani huku wakisongamana katika vituo vya burudani na matatu.

Data iliyotolewa na Wizara ya Afya, inaonyesha kuwa kufikia Alhamisi, Kaunti hiyo ilirekodi visa vipya 29.

Jumla ya visa vya Covid-19 mjini Uasin Gishu imepita ile ya baadhi ya kaunti zilizotangazwa kama “Kaunti Zinazosemekana kuwa na Maambukizi Mengi.”

Idadi yake kwa sasa ni 4,865 ambayo ni zaidi ya Machakos (4,438) na Kajiado (4,253).

Haya yamejiri baada ya Kamishna wa Kaunti, Bw Stephen Kihara na Waziri wa Afya Evelyn Rotich, kukutana na machifu Alhamisi kwa lengo la kuimarisha sheria za kudhibiti virusi vya corona. Bw Kihara aliagiza machifu na vyombo vingine vya usalama kuhakikisha kuwa kanuni za Covid-19 zinazingatiwa na raia wote.

“Tunataka kusisitiza kwamba tutaendelea kutekeleza amri za rais na mikakati ya kuzuia ili kupunguza maambukizi ya Covid-19,” alisema afisa huyo.

Gavana Jackson Mandago alitoa wito kwa wakazi eneo hilo kuwajibika binafsi kufuata kanuni za kudhibiti maambukizi ya Covid-19.

Gavana Mandago alielezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa visa vya maambukizi kote katika Kaunti hiyo.

Kulingana na gavana huyo, Kaunti hiyo ni ya pili katika maambukizi ya COVID-19 baada ya Nairobi ambapo aliwahimiza wakazi kujukumika binafsi ili kujikinga.

“Dalili nyingi za kawaida tunazozifahamu ni kama vile homa, joto jingi, kupoteza uwezo wa kunusa,” alisema Bw Mandago. Naibu Gavana Daniel Chemno alionya kuwa wagonjwa wengi wa Covid-19 wamegeukia kujitibu wenyewe manyumbani mwao.

“Wanajitibu dalili mbalimbali kama vile kuendesha na kuwa na joto jingi mwilini hali inayoishia kuwa matatizo hatari kiafya. Nataka kuwaeleza wakazi wetu kutafuta matibabu mapema katika vituo vya afya vilivyo karibu,” alisema Bw Chemno, baada ya mkutano wa dharura na maafisa wa usalama na wadau wengine kwa lengo la kubadilisha mikakati.

Kufikia Aprili 10, kulikuwa na wagonjwa 27 kwenye vitanda vya ICU na wengine zaidi ya 85 waliolazwa katika vituo vya afya mbalimbali katika kaunti hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Ngara Sportiff kujikaza kiume kumaliza kileleni

Shalom Yassets inavyookoa vijana mitaani