• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2024 2:01 PM
Ngara Sportiff kujikaza kiume kumaliza kileleni

Ngara Sportiff kujikaza kiume kumaliza kileleni

Na JOHN KIMWERE

NI kweli wahenga hakupata mafuta kwa mgongo wa chupa walipoketi na kulonga kuwa ‘Lisolokuwapo moyoni pia machoni halipo.’ Ni msemo unaoashiria kwamba hakuna lolote linaloweza kutimia bila ya kufanyiwa kazi.

Aidha unafundisha wanadamu kuwa ili kufikia mafanikio yoyote ni lazima wahusika wazamie mpango mzima kuwawezesha kuibuka na mkakati kabambe bila kusahau kujiwekea maazimio yote wanayolenga kufikia.

Katika jukwaa la michezo, msemo huo unahimiza wachezaji kukaza mwendo na kufahamu kiwango wanacholenga kutimiza kufikia kilele cha mafanikio yao. Ndivyo wanavyosaidiki wachana nyavu wa Ngara Sportiff ambayo hushiriki mechi za Kundi A kuwania Ligi ya Wilaya katika Tawi la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) la Nairobi West.

”Katika mpango mzima tunalenga kujituma kiume kuhakikisha tunafanya kweli kwenye kampeni za msimu huu lengo kuu likiwa kumaliza kileleni na kutwaa tiketi ya kupandishwa ngazi,” alisema kocha wa Ngara Sportiff, Stephen King’ori na kutoa wito kwa wachezaji wake kutolaza damu dimbani kwenye kampeni zao.

Anadokeza kuwa ana wachezaji wazuri wenye uwezo wa kufanya kweli kwenye kampeni za ngarambe ya muhula huu. Kocha huyo anasema kwamba wanajipatia muda wa miaka sita hivi kuhakikisha wamefuzu kushiriki ngarambe ya Ligi Kuu nchini.

Kikosi hicho chini ya nahodha, Jato Odingo na mwenzake Abraham Omole kinajivunia kuwa kati ya tatu bora katika jedwali la kipute hicho kwa kuzoa alama sita baada ya kushiriki mechi tatu.

Katika msimamo wa kipute hicho, Derby FC inaongoza kwa kuzoa tisa, sawa na Huruma Sports Club baada ya kila moja kucheza mechi tatu.

Timu hii inajivunia kukuza wachezaji kadhaa waliofanikiwa kujiunga na vikosi zingine akiwamo Edward Ogeso (Barclays), Clement Ochola (Housing Finance Corporation FC), Robert Shibutse aliyechezea Farmers Choice FC, Blue Triangle, Carnivore FC na Hakati FC. Pia yupo Louis Otieno (Ujuzi FC).

Hata hivyo ana hofu kwa kuzingatia baadhi ya wapinzani wao wameonesha wazi kuwa wamejipanga kiume kushusha upinzani wa kufa mtu. Kocha huyo ametaja kuwa baadhi ya klabu zinazoweza kuzima ndoto yao kama Huruma Sports, Derby FC na King Power kati ya zingine.

Ngara Sportiff iliyoanzishwa mwaka 1985 hufanyia mazoezi katika Uwanja wa New Ngara Estate, Nairobi. Nahodha wake anatoa wito kwa wenzake kuendelea kushiriki mazoezi ya kibinafsi katika kipindi hiki ambapo serikali imesitisha shughuli za michezo nchini kwenye juhudi za kuzuia msambao wa virusi vya corona vinavyochangia ugonjwa kwa Covid-19.

Klabu hii inajumuisha wachezaji kama: Abraham Omole(naibu wa nahodha), Fardeen Khan, Faheem Velle,Ayman Hussein, Ali Hussein, Twahir Suleiman, Vincent Oduori, Joseph Mumo, Benson Kipino, Benjamin Parmet,Mike owino, Andrew Omollo, Tofik Hussein, Paul Omulupi, Stephen Omondi, Jato Odingo(nahodha),Stephen Kariuki na Jeff Jysell.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool waafikiana na RB Leipzig kumsajili beki Konate...

Covid: Raia lawamani kwa kupuuza kanuni