• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
CRA yashauri kaunti kutengewa Sh370b mwaka 2022

CRA yashauri kaunti kutengewa Sh370b mwaka 2022

Na LEONARD ONYANGO

MAGAVANA wamepata pigo baada ya Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) kukataa wito wao wa kutaka fedha zinazotolewa kwa serikali za kaunti ziongezwe kutoka Sh370 bilioni hadi Sh381 bilioni.

Tume ya CRA jana ilipendekeza serikali za kaunti zitengewe Sh370 bilioni katika mwaka wa fedha ujao wa 2022/2023.

Kulingana na tume hiyo inayoongozwa na Bi Jane Kiringai, nchi inakabiliwa na changamoto tele za kiuchumi ‘hivyo haiwezekani kwa serikali za kaunti kupewa Sh381 bilioni.’

“Nchi inatarajiwa kupata mapato ya Sh2.14 trilioni mwaka 2022. Serikali ya kitaifa itasalia na Sh1.76 trilioni na serikali za kaunti zitapewa Sh370 bilioni,” inasema ripoti ya CRA.

Tume hiyo inasema janga la corona limetatiza ukuaji wa uchumi na kiasi kikubwa cha mapato kitatumika kutoa usalama katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 na kulipa madeni ambayo Kenya inadaiwa.

Bi Kiringai alionya kuwa nchi huenda ikalazimika kukopa zaidi iwapo ombi la magavana la kutaka kuongezewa mgao wa fedha litazingatiwa.

Baraza la Magavana (CoG) mwezi Oktoba, lilikataa pendekezo la CRA kutaka wapewe Sh370 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Magavana walisema sababu zilizotolewa na CRA hazikuwa na mashiko.

Kaunti zilipewa Sh370 bilioni katika mwaka huu wa fedha (2021/2022) ikilinganishwa na Sh316.5 bilioni miaka iliyopita.

Iwapo pendekezo hilo la CRA litapitishwa, Kaunti za Nairobi, Nakuru, Turkana na Kakamega zitajipatia kitita kikubwa cha Sh19.3 bilioni, Sh13 bilioni, Sh12.6 bilioni na Sh12.4 bilioni mtawalia, mwaka ujao wa 2022.

Kaunti ambazo zitapokea kiasi kidogo ni Lamu Sh3.1 bilioni, Tharaka Nithi (4.2 bilioni), Elgeyo Marakwet (4.6 bilioni) na Isiolo (4.7 bilioni).

Ripoti ya CRA pia ilifichua kuwa, kaunti 35 zinakiuka sheria inayotaka serikali za kaunti kutumia angalau asilimia 30 ya fedha zinazopata kutoka kwa serikali ya kitaifa katika miradi ya maendeleo.

You can share this post!

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika shule ya...

KINA CHA FIKIRA: Elimu bila nasaha kwa wanafunzi ni bomu...

T L