• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika shule ya Msingi ya Mutweamboo, Makueni

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika shule ya Msingi ya Mutweamboo, Makueni

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Mutweamboo (CHAKIMU) kina malengo ya kuchangia makuzi ya Kiswahili, kubadilisha mtazamo hasi wa wanafunzi kuhusu Kiswahili, kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kuboresha matokeo ya KCPE Kiswahili.

Mbali na kuwa daraja la kuwavusha watahiniwa katika masuala ya kiakademia, madhumuni mengine ya chama hiki ni kuwapa wanafunzi jukwaa mwafaka la kukuza vipaji vyao vya uigizaji, utunzi wa mashairi, uandishi wa kazi bunilizi, utambaji wa hadithi na uchoraji.

Shule ya Msingi ya Mutweamboo inapatikana katika kaunti ndogo ya Mukaa, eneo la Kasikeu, Kaunti ya Makueni na ilianzishwa mnamo 1938 kwa udhamini wa Kanisa la African Inland Church (AIC). Kwa sasa iko chini ya uongozi wa Mwalimu Mkuu Bw Shadrack Musau akisaidiana na Naibu Mwalimu Mkuu, Bw Daniel Muteti na Mwalimu Mwandamizi Bi Bernadine Musyoka.

Walimu wanaosukuma gurudumu la Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Mutweamboo ni Bw Harrison Musyoka, Bw Ndolo, Bi Lilian na Bi Elizabeth.

Kupitia kaulimbiu ‘Comitted to Excellence’, Shule ya Msingi ya Mutweamboo imefaulu kuwaunganisha wanafunzi wote shuleni na kuwatia azma ya kufaulisha nyingi za ndoto zao katika siku za halafu.

Zaidi ya kutoa nafasi kwa wanafunzi kutotonoa talanta na vipaji vyao, CHAKIMU pia kimewapa wanafunzi jukwaa zuri la kuelekezana ipasavyo, bila usaidizi wa walimu wao kila mara, katika baadhi ya mada zinazowatatiza madarasani.

Walimu na wanafunzi pia wanajivunia usomaji wa mara kwa mara wa magazeti ya ‘Taifa Leo’ kupitia mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG).

Kupitia mradi huo uliozinduliwa rasmi katika Shule ya Msingi ya Mutweamboo wiki hii, NMG inatumia magazeti ya ‘Taifa Leo’ kuimarisha viwango vya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili na masomo yote mengine katika shule za humu nchini.

Kwa mujibu wa Bw Musau, wengi wa wanafunzi wake wanaothamini na kuchangamkia usomaji wa ‘Taifa Leo’ hudumisha umahiri wao katika lugha kwa kukwangura alama za juu zaidi katika mitihani ya kitaifa (KCPE).

Anaungama kwamba majaribio ya mitahini katika ‘Taifa Leo’ ni daraja halisi la mafanikio kwa wengi wa wanafunzi wake ambao wamechochewa kutia fora katika somo la Kiswahili.

Wanafunzi 95 waliotahiniwa kutoka Shule ya Msingi ya Mutweamboo katika KCPE 2020 walifaulu vyema kwa kusajili alama wastani ya 306.40. Mwanafunzi wa kwanza alizoa alama 399 na akawa miongoni mwa wanne kutoka shuleni humo waliojiunga na shule za kitaifa za Kathiani Girls, Makueni Boys na St Mary’s Egoji kwa masomo ya sekondari.

Shule ya Msingi ya Mutweamboo kwa sasa ina watahiniwa 93 wanaolenga kusajili alama wastani ya 310 katika KCPE 2021 chini ya uelekezi wa walimu 16.

You can share this post!

Wakazi walaumiwa kuficha al-Shabaab

CRA yashauri kaunti kutengewa Sh370b mwaka 2022

T L