• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Diwani ndani miaka minane kwa kujaribu kuokoa watu waliohukumiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya

Diwani ndani miaka minane kwa kujaribu kuokoa watu waliohukumiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya

Na KALUME KAZUNGU

DIWANI wa Wadi ya Mkomani, Kaunti ya Lamu, Yahya Ahmed Shee, maarufu Basode, huenda akapoteza kiti chake baada ya Jumatano mahakama kumhukumu kifungo cha miaka minane na pia kumpiga faini ya Sh800,000.

Mwakilishi huyo wa Wadi Alhamisi wiki iliyopita alipatikana na hatia ya makosa sita aliyotekeleza mwaka 2017, ikiwemo kujaribu kuwaokoa watu watatu waliokuwa wamehukumiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Lamu, Allan Temba alisema korti imemhukumu Basode miaka minne gerezani kwa makosa matatu ya kwanza.

Makosa hayo ni pamoja na tukio ambapo diwani huyo kwa ushirikiano na wenzake walijaribu kumuokoa kwa lazima Zamzam Mohamed Salim ambaye alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 20 gerezani kwa ulanguzi wa mihadarati mnamo Juni 2, 2017.

Kosa lingine alilopatikana kuwa na hatia ni lile la kujaribu kumuokoa mfungwa, Ali Mzee Ali tarehe iyo hiyo ya Juni 2, 2017 ambaye pia alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani kwa kulangua dawa za kulevya.

Kosa la tatu ni la kujaribu kumuokoa mfungwa mwingine kwa jina Nyathumani Yusuf ambaye alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani.

Bw Temba alisema kwa sababu makosa hayo matatu yalitekelezwa wakati mmoja, mhukumiwa atafungwa jumla ya miaka minne.

Katika kosa la nne na la tano, ambapo Basode alipatikana na hatia ya kuwazuia polisi kutekeleza jukumu lao na kujaribu kuwazuia na kuwakataza kutekeleza majukumu yao ya kisheria, korti ilimhukumu kifungo cha miaka mingine minne gerezani au faini ya Sh800,000.

Katika kosa la sita ambapo diwani alikuwa amepatikana na hatia ya kushiriki maandamano yasiyo halali nje ya korti mnamo Juni 2, 2017, korti ilimhukumu miaka 18 gerezani.

Upande wa mashtaka ulikuwa umewakilishwa na Afisa Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP), Eddie Kaddede na Kagenyo Kiongo ambao wote walitaja hukumu hiyo kuwa ya haki hasa katika utekelezaji na kuheshimiwa kwa sheria za nchi na utawala.

Basode alikuwa amewakilishwa na mawakili, Afred Omwancha na Kenneth Njuguna ambao wote walisema watawasilisha rufaa kwenye mahakama za Kenya kupinga hukumu hiyo.

Diwani huyo kwa sasa amefungwa kwenye gereza la umma la Hindi.

Ana haki ya kukata rufaa katika kipindi cha siku 14 zijazo.

You can share this post!

Serikali ya Mwangi Wa Iria yatamatisha utoaji wa kilo...

Jinsi NMS inavyojikakamua kuangazia usalama wa waendao kwa...