• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
EACC kutwaa mali ya wenye vyeti ghushi

EACC kutwaa mali ya wenye vyeti ghushi

NA KNA

TUME ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC) imeahidi kuwa itatwaa pesa na mali kutoka kwa wale ambao walitumia vyeti ghushi kuwania na kushinda vyeo vya uongozi katika uchaguzi mkuu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak alisema kuwa hivi karibuni, EACC itaanza kutwaa mali ya wanasiasa ambao walinufaika na mshahara unaofungamana na vyeo vyao ilhali walitumia vyeti ghushi kupata nafasi hizo za uongozi.

“Tume hii itakuwa na subira hadi mkondo wa kisheria ukamilike kwa wale ambao wameghushi vyeti vya masomo na kuishia kushinda viti walivyoviwania. Iwapo watapatikana na hatia, tutahakikisha kuwa pesa zote walizolipwa kama mishahara na marupurupu zinarejeshwa. Hii itajumuisha kutwaa mali yao kufidia pesa hizo,” akasema.

Bila kufichua idadi ya viongozi waliochaguliwa ambao wanafuatiliwa na EACC kwa kughushi vyeti vya masomo, Bw Mbarak alisema kuwa kuna kesi nyingi mbele yake ambazo zinawahusisha wanasiasa na pia viongozi wa serikali na wale wa mashirika ya umma.

Hata hivyo, alifichua kuwa magavana wawili wanaohudumu kwa sasa ni kati ya wale ambao wana kesi kuhusu madai ya kughushi vyeti vya masomo kortini.Hivi majuzi, EACC iliwakamata na kuwashtaki waliokuwa Makamishina wa Ardhi Wilson Gachanja na Zablon Mabeya pamoja na aliyekuwa mkuu wa kitengo cha mpangilio jijini Jabu Salim Mohamed kuhusiana na ufisadi ambao wanadaiwa walishiriki mnamo 1994.

Bw Mbarak alisisitiza kuwa watumishi wa umma na viongozi waliochaguliwa watawajibikia ufisadi ambao walishiriki wakiwa afisini.

Aliongeza kuwa EACC imetwaa mali ya mabilioni ya fedha iliyopatikana kwa njia haramu kutoka kwa wanasiasa waliostaafu na watumishi wa umma na pia kuna wengine wengi ambao pia bado wanachunguzwa.

“Baadhi walikiri makosa ya uhalifu waliyoyatenda na kuomba kurejesha mali kwa walipaji ushuru na tumetumia mkondo mwingine wa kutatua mizozo kupata pesa za umma zilizoibwa na mali,” akaongeza huku akisema kuwa wapo radhi kupambana na ufisadi na kutwaa mali iliyoibwa hata kesi zikichukua miaka na dahari kortini.

“EACC haimakinikii kuwa kesi imechukua miaka mingi tangu iwasilishwe mahakamani. Wale ambao walishikilia vyeo vya juu vya uongozi watalipia vitendo vyao vya ufisadi hata baada ya kustaafu,” akasema.

Afisa huyo alisema kuwa kwa sasa wanaendeleza uchunguzi kuhusu kesi kadhaa ambapo baadhi ya watu wamelaumiwa kuiba mali ya umma hasa kipindi hiki ambacho ni cha mpito.

“Wizi huu unafanyika kupitia kubuni nafasi za ajira kiharamu na pia bajeti kwa miradi hewa ambayo haitekelezwi. Tuko katika kipindi cha mpito lakini lazima tuwajibikie matumizi ya fedha badala ya kutumia mwanya huo kuiba,” akasema huku akiongeza kuwa wale watakaopatikana wameiba watakabiliwa kisheria.

  • Tags

You can share this post!

Aliyekuwa kipa nguli wa Rangers na timu ya taifa ya...

Ruto amlima Uhuru waziwazi

T L