• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 3:59 PM
Ruto amlima Uhuru waziwazi

Ruto amlima Uhuru waziwazi

CHARLES WASONGA Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto sasa ameamua kumshambulia moja kwa moja mkubwa wake, Rais Uhuru Kenyatta akimlaumu kwa changamoto za kiuchumi zinazoikumba nchi hii.

Hii inaonekana kama mkakati wake mpya wa kujiongezea umaarufu miongoni mwa wapigakura muda ukiyoyoma kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kwa miaka minne ambayo amekuwa akiendesha kampeni zake, Dkt Ruto amekuwa akiepuka kumtaja au kumshambulia Rais Kenyatta moja kwa moja.

Hata hivyo, katika siku chache zilizopita, Dkt Ruto amekuwa akisisitiza kuwa Rais Kenyatta ndiye anayepaswa kulaumiwa binafsi kwa kero la kupanda kwa gharama ya maisha, akisema chimbuko la kero hilo ni handisheki kati yake na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Ishara kuwa Dkt Ruto ameamua ‘kufungua mkono’ dhidi ya Rais Kenyatta zilijitokeza wazi Jumatano alipolaumu Serikali kwa kujenga kiwanda cha kutengeneza bunduki badala ya kuanzisha cha kutengeneza nguo kinachoweza kuajiri vijana wengi.

Katika ishara inayoibuka kama mkakati aliokuwa ameweka, siku iliyotangulia, vinara wa muungano anaoongoza wa Kenya Kwanza, wakiongozwa na kinara wa ANC, Bw Musalia Mudavadi, waliwahusisha Rais na Bw Odinga na kile walichokitaja kama njama ya kuuza bandari za Mombasa, Lamu, Naivasha na Kisumu kwa kampuni moja ya Dubai, kinyume cha sheria.

“Bei ya unga imepanda hadi Sh230 kwa paketi moja kwa sababu ya wewe Rais kumleta huyu mzee wa kitendawili ndani ya serikali. Handisheki yenu ndiyo imevuruga ajenda nne kuu za maendeleo na waacha mamilioni ya Wakenya wakihangaika,” Dkt Ruto akawaambia wafuasi wake Jumamosi mjini Chuka, Tharaka Nithi.

Katika kumshambulia Rais anayeunga mpinzani wake mkuu Bw Odinga, Dkt Ruto anasisitiza kuwa Kiongozi wa Nchi anapaswa kuwajibika kibinafsi kwa hali inayokumba nchi kwa kumtenga katika serikali na kukumbatia Kiongozi wa Upinzani.

Vilevile, akizindua manifesto yake mnamo Alhamisi uwanjani Kasarani, Nairobi, Naibu Rais aliahidi kuunda majopo kadhaa kuchunguza sakata mbalimbali zilizofanyika chini ya utawala wa Rais Kenyatta na kudhoofisha uchumi.

Dkt Ruto ameachilia ‘mishale’ yake waziwazi kumlenga Rais Kenyatta kiasi cha kumwambia astaafu na kutazama aone nchi inavyoendeshwa vyema chini ya serikali ya Kenya Kwanza iwapo muungano huo utashinda urais na kuunda serikali.

Jana Jumamosi alimwambia Rais wazi kuwa hafai kumlaumu kwa shida zinazokumba Wakenya na kumtaka abebe msalaba wake.

“Uliniambia ulitaka kufanya kazi na wengine, nilikupa nafasi. Kwa hivyo, kwa nini unanilaumu kwa shida zinazokumba Wakenya?” alihoji Dkt Ruto.

“Baada ya Rais Kenyatta kumwingiza yule mzee wa vitendawili (Raila) serikalini kupitia handisheki, miradi ya maendeleo ilisitishwa na wakatuletea BBI na reggae,” Dkt Ruto akasema Ijumaa alipohutubia msururu wa mikutano ya kampeni katika Kaunti ya Embu.

Awali, Dkt Ruto hakuwa akitaja jina la rais japo amekuwa akikosoa mchakato wa kubadilisha katiba kupitia BBI.

Jana Jumamosi, Dkt Ruto, na wandani wake, waliendelea kumshambulia Rais Kenyatta wakiwa Tharaka Nithi, wakidai Kiongozi wa Nchi alisaliti eneo la Mlima Kenya kwa kuamua kumuunga Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais mwaka huu.

USALITI

Seneta wa kaunti hiyo, Prof Kithure Kindiki alishutumu Rais kwa kumsaliti Dkt Ruto na wafuasi wa Jubilee ambao walimpigia kura kwa wingi katika chaguzi za miaka ya 2013 na 2017.

“Usaliti huu ulianza baada ya sisi kumchagua Uhuru kwa muhula wa pili. Alimweka kando Naibu Rais na kumteua na akamteua Raila kuchukua nafasi hiyo. Kwa hivyo, hatuwezi kuwajibikia makosa ya muhula wa pili,” akasema Prof Kindiki.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi wanasema kuwa Ruto ameamua kumshambulia moja kwa moja Rais Kenyatta, hasa katika eneo la Mlima Kenya ili kukabiliana na mawimbi ya Azimio la Umoja katika ngome hiyo.

“Aidha, kwa sababu huu ni mkondo wa lala salama katika kampeni za kuelekea Agosti 9, Ruto anataka kujiondolea maovu yote yanayohusishwa na utawala huu, japo angali anashikilia kiti cha Naibu Rais,” anasema Bw Mark Bichachi.

“Hii ndio maana anadai chimbuko la shida ya kupanda kwa gharama ya maisha ni handisheki huku akihusisha Rais Kenyatta na Bw Odinga na madai ya kuuzwa kwa bandari zake,” anaongeza.

  • Tags

You can share this post!

EACC kutwaa mali ya wenye vyeti ghushi

Ajali yaangamiza 3 akiwemo mke wa aliyekuwa mbunge

T L