• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
EACC yammulika gavana wa Lamu

EACC yammulika gavana wa Lamu

Na LEONARD ONYANGO

TUME ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) imependekeza kushtakiwa kwa Gavana Fahim Twaha wa Lamu, kwa kukiuka kanuni za uajiri wa watumishi wa Umma.

Tume hiyo imekuwa ikichunguza madai kuwa Bw Twaha aliajiri wafanyakazi 12 wa kaunti bila kuzingatia kanuni za uajiri.

EACC tayari imekamilisha uchunguzi wake na kukabidhi faili kwa ofisi Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ili iweze kuamua iwapo gavana huyo atakamatwa na kushtakiwa.

Kulingana na ripoti hiyo, Gavana Twaha akishirikiana na Katibu wa Kaunti ya Lamu na Mkuu wa Utumishi wa Umma walitoa barua za uajiri kwa watu 12 katika vyeo tofauti.

“Uchunguzi uligundua kuwa watu hao 12 walioajiriwa hawakuwa wamehitimu kielimu na pia waliajiriwa bila kuhusisha Bodi ya Huduma za Kaunti, ambayo imepewa jukumu la kuajiri wafanyikazi wa serikali ya kaunti,” inadokeza sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo ilikabidhiwa DPP mnamo Agosti 21, 2021 ikipendekeza kuwa Gavana Twaha na maafisa waliotajwa washtakiwe kwa makosa 12 ya utumizi mbaya wa ofisi zao.

Kwingineko, EACC imependekeza kushtakiwa kwa maafisa wa Mamlaka ya Bandari (KPA) pamoja na wakurugenzi wa kampuni sita za kibinafsi kwa madai ufisadi katika ununuzi wa maji ya kunywa yaliyosababisha kupotea kwa Sh137.6 milioni.

Tume hiyo inasema ufisadi huo uliohusisha kampuni sita zilizopewa kandarasi ya kuuzia KPA maji bila kufuata kanuni za ununuzi ulifanyika katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.

EACC inaeleza kuwa uchunguzi wake uligundua baadhi ya kampuni husika zililipwa licha ya kuwa hazikuwasilisha maji kwa KPA.

Kampuni zilizotajwa na EACC kwa madai ya kuhusika katika sakata hiyo ni Sammix Enterprises, Mombasa Fresh Water Supply Company, Pincho Traders, Smech Enterprises, Nyavu Traders na Aquisana Limited.

EACC kwenye ripoti yake iliyowasilishwa kwa DPP ili kuwachukulia hatua washukiwa inasema imependekeza wafunguliwe mashtaka ya udanganyifu, matumizi mabaya ya ofisi, kukaidi sheria na kanuni za ununuzi na ulaghai wa mali ya umma.

KPA pia imemulikwa na EACC kuhusiana na utoaji zabuni ambayo gharama yake imezidi kiasi cha pesa zilizotengwa kwenye bajeti.

Tume hiyo inasema kampuni ya Alootek Systems Limited ilipewa zabuni hiyo ya kutunza mtambo wa Copco Compressors ya thamani ya Sh8.4 milioni.

Inasema Alootek ilipewa zabuni hiyo moja kwa moja bila kuitisha maombi kutoka kwa kampuni nyingine.

Sasa EACC inataka maafisa wa KPA waliohusika pamoja na wakurugenzi wa Alootek washtakiwe.

You can share this post!

Wataka suti tu!

Korti yapatia serikali kibali kutwaa jumba la aliyeuawa

T L