• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Wataka suti tu!

Wataka suti tu!

ONYANGO K’ONYANGO NA LEONARD ONYANGO

WANASIASA wakuu wanaomezea mate urais mwaka ujao wamesisitiza kuwa sharti walio katika mirengo yao wawanie viti tofauti kwa vyama wanavyoongoza vya UDA na ODM.

Hatua hii imewaweka katika hali ya mvutano na vyama vidogo ambavyo vinataka kuwa na mwafaka ambapo vitakuwa na wagombeaji wao.

Lakini vigogo wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga, wamesimama kidete kupinga vyama washirika wao kuwa na wagombeaji.

Wanasiasa hao wanashinikiza wafuasi wao kuwapigia kura wawaniaji wa urais, ugavana, useneta, mwakilishi wa wanawake, mbunge na diwani wa vyama vyao pekee.

Hapo jana Odinga aliwataka wafuasi wake kuchagua wagombea wa chama hicho kutoka udiwani hadi urais.

Bw Odinga alionya kuwa wawaniaji wa vyama vingine pamoja na wale wa kujitegemea wakishinda katika uchaguzi ujao wataweka ODM katika hatari ya kukosa pesa ambazo hutolewa na serikali kwa vyama vya kisiasa.

“Hao wawaniaji wa kujitegemea wanasababisha chama kukosa fedha ambazo hutolewa kwa vyama vya kisiasa kutoka kwa serikali. Fedha hizo hutolewa kulingana na idadi ya kura ambazo chama kimepata,” akasema Bw Odinga.

Aliwataka wanasiasa walio na nia ya kuhama chama hicho wakishindwa katika kura za mchujo waondoke chamani sasa.

Dkt Ruto anasema kuwapigia kura wawaniaji wa UDA katika nafasi zote sita za uongozi kutahakikishia wafuasi wake wamejitokeza kwa wingi kumpigia kura ya urais.

Sababu nyingine ya kupenda suti ni kuwa iwapo duru ya pili ya uchaguzi wa urais itafanyika, hawatakuwa na wasiwasi wa wabunge waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama vingine kuhamisha uaminifu wao kwa mpinzani.

Hatua hiyo pia inakusudiwa itazima vyama vidogo kudai mgao mkubwa wa vyeo katika serikali zao iwapo watashinda.

Kuzuia migawanyiko

Suala lingine wanaloangaziwa na viongozi hao ni kuwa wakishinda watahakikishiwa udhabiti na kuzuia migawanyiko katika serikali zao, kwani ndio watakuwa na usemi mkuu wa vyama wanavyomiliki. Hii pia itawasaidia kupitisha sera za utawala wao katika mabunge ya kitaifa na Seneti kwa urahisi.

Seneta wa Bomet, Dkt Christopher Lagat, Alhamisi alisema kuwa kushinda viti vyote kwa tiketi ya chama kimoja kutawaepushia vyama vidogo au wanasiasa ambao watawawekea masharti makali baada ya uchaguzi.

“Miungano huwa na changamoto zake na washirika wako wanaweza kukuacha wakati unawahitaji zaidi kutokana na maslahi yao ya kibinafsi,” akasema Dkt Lagat.

Mwanasiasa huyo alisema ni vyema UDA kisake nafasi za uongozi kivyake na iwapo kitalemewa na kura za urais katika duru ya kwanza, hapo ndipo watawasaka washirika wapya na kuingia kwenye muungano.

“Kuungana na vyama vingine kabla ya kura kuna masharti yake na kutatuharibia hesabu iwapo kura itarudiwa kwa sababu washirika wapya nao watataka tuwatimizie maslahi yao ilhali tayari tuna muungano,” akaongeza.

Kauli hiyo iliungwa mkono na wabunge David Rono (Keiyo Kusini) na Rigathi Gachagua wa Mathira ambao walisema wana matumaini ya kuunda serikali ijayo na chama hicho hakina haja ya kuingia kwenye muungano wowote kwa sasa.

UDA hasa kinalenga kushinda viti vingi eneo la Mlima Kenya na Bonde la Ufa.

“Sisi hatutaki ‘handisheki’ kama ya Uhuru na Raila bali tutazama na kuendesha kampeni kali kote nchini ili tupate viongozi wengi. Nina hakika tutakuwa na wawakilishi wengi kwenye mabunge yote kote nchini,” akasema Bw Gachagua.

Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen naye alisisitiza kwamba UDA itahakikisha kuwa wanasiasa watakaochaguliwa ni wale waaminifu kwa chama hicho.

Kando na UDA, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula amewataka wakazi wa Bungoma na Trans Nzoia wawapigie kura wanasiasa wa Ford Kenya pekee.

Naye Musalia Mudavadi wa ANC amewataka wapigakura kutoka Magharibi wawachague wawaniaji wa ANC pekee, mbinu ambayo inalenga kuvifungia vyama vingine nje ya eneo hilo.

You can share this post!

Michael Carrick aondoka Man-United baada ya kusimamia klabu...

EACC yammulika gavana wa Lamu

T L