• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Eneobunge lisilo na hata inchi moja ya lami tangu uhuru

Eneobunge lisilo na hata inchi moja ya lami tangu uhuru

NA KALUME KAZUNGU

HUKU maeneo mengi ya Kenya yakijivunia kuboreshwa kwa miundomsingi ikiwemo barabara, reli ya kisasa, viwanja vya ndege na mengineyo, kwa wakazi wa eneobunge la Lamu Mashariki hali ni tofauti.

Kwa karibu miaka 60 sasa tangu uhuru wa nchi hii kupatikana, wakazi wa eneobunge hilo hawajabahatika kuwa na angalau kilomita, mita, sentimita wala hata inchi moja ya barabara ya lami kinyume na sehemu zingine.

Barabara zipatikanazo eneo hilo ni zile za vumbi wakati wa kiangazi na matope msimu wa mvua.

Mbali na kukosekana kwa lami, barabara hizo pia zimesheheni mashimo, hali ambayo hulazimu wanaozitumia kuwa waangalifu wakiendesha magari, pikipiki na baiskeli kwa mwendo wa konokono wasijipate wakihusika kwenye ajali na hata maafa.

Lamu Mashariki inajumuisha karibu visiwa 15 kati ya 35 vipatikanavyo Kaunti ya Lamu.

Miongoni mwa visiwa vipatikanavyo eneo hilo ni Faza, Kizingitini, Siyu, Ndau, Kiwayu, Mkokoni, Kiunga, Pate, Tchundwa, Mbwajumwali, Mtangawanda, Shanga, Rubu na viunga vyake.

Eeneobunge la Lamu Mashariki limegawanywa kwa wadi tatu ambazo ni; Kiunga, Faza na Basuba-Msitu wa Boni, ambazo zote zinakosa barabara ya lami.

Kulingana na sensa ya mwaka 2019, Lamu ina jumla ya watu 143,920 ambapo zaidi ya watu 22,000 wanapatikana Lamu Mashariki huku idadi iliyobakia ikipatikana Lamu Magharibi.

Licha ya watu kuishi Lamu Mashariki, wakiwemo wafanyakazi wa umma, serikali kuu imeendelea kutelekeza eneo hilo kimiundomsingi, hasa barabara.

Akizungumza kisiwani Faza, Mbunge wa eneo hilo, Ruweida Obo aliiomba serikali kuzingatia kujenga barabara na kuweka lami ili wakazi wajihisi kuwa Wakenya.

Mbunge wa Lamu Mashariki Ruweida Obo katika mahojiano na Taifa Leo. PICHA | KALUME KAZUNGU

“Inavunja moyo kuona kwamba katika karne ya 21 na karibu miaka 60 sasa ya uhuru wa nchi hii imepita bila ya eneobunge langu kuwa na angalau futi moja ya barabara yenye lami. Walinda usalama wanaohudumia eneo hili wanakumbwa na matatizo ya magari kuharibika ovyo ovyo. Ni vyema serikali itujengee barabara ya lami ili uchukuzi urahisishwe. Hilo likifanyika, usalama utaboreshwa kwani maafisa wanaoshika doria watakuwa wanazunguka kiurahisi,” akasema Bi Obo.

Mbali na tatizo la barabara, baadhi ya vijiji au visiwa vya Lamu Mashariki vinakosa mawimbi ya mawasiliano, hasa yale ya simu za mkononi.

Wakazi wa vijiji au visiwa kama vile Siyu, Mkokoni, Madina na baadhi ya vijiji vilivyoko msitu wa Boni wanaishi gizani kwa kukosa mawimbi ya mawasiliano, hivyo kuwatenga au kuwazuia kuchangia mijadala muhimu ya kitaifa, hasa kwenye mitandao ya kijamii.

Ahmed Athman, mkazi wa Mkokoni anaiomba serikali kuzingatia kuwajengea minara ya mawasiliano ili kuwawezesha kuunganika na Wakenya wengine kupitia mawasiliano ya simu na mitandao ya kijamii.

“Tuko na shida kubwa ya kukosa mawimbi ya mawasiliano. Mijadala inatupita hivyo mitandaoni. Licha ya karne za sasa kuwa za utandawazi kutokana na mawasiliano yaliyoboreshwa, sisi wakazi wa Mkokoni na Lamu Mashariki bado tunaishi zama za giza kwa kukosa miundomsingi ya kuwasiliana. Serikali itukumbuke. Sisi pia ni Wakenya,” Bw Athman akaambia Taifa Leo kupitia mahojiano ya kipekee.

Ng’ombe wakitembea kwenye barabara ya Mtangawanda kuelekea Faza, Lamu Mashariki ambayo ni ya vumbi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wakazi pia walisisitiza haja ya taasisi za kifedha, hasa benki kufungua matawi yao eneo la Lamu Mashariki ambalo linakosa huduma hizo.

“Tunalazimika kuhifadhi fedha zetu kwenye mashimo ardhini ndani ya nyumba zetu kwani hatuna benki za kutrsaidia kuweka. Watuletee benki,” akasema Bw Titi Mbwana, mkazi wa Tchundwa, Lamu Mashariki.

  • Tags

You can share this post!

Majogoo wa jiji Sakaja na Babu Owino wapapurana siku nzima,...

Kichuna Huddah Monroe asema Ruto atakuwa rais mbovu zaidi...

T L