• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Majogoo wa jiji Sakaja na Babu Owino wapapurana siku nzima, kampeni za 2027 zimeanza?

Majogoo wa jiji Sakaja na Babu Owino wapapurana siku nzima, kampeni za 2027 zimeanza?

NA WANDERI KAMAU

WANASIASA tofauti nchini wanaonekana kuanza kampeni za mapema kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027, wengi sasa wakianza kuwakosoa wenzao wanaoshikilia nyadhifa wanazomezea mate.

Baadhi yao pia wanajisawiri kama “watetezi wa raia”, wadadisi wakitaja hilo kama mbinu za mapema kuanza kujitayarisha kwa uchaguzi huo.

Baadhi ya wale wanaoonekana kuanza kampeni zao za mapema ni mbunge Babu Owino (Embakasi Mashariki) dhidi ya Gavana Johnson Sakaja wa Nairobi na Waziri wa Biashara Moses Kuria dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Mnamo Jumapili, Septemba 17, 2023, Bw Owino na Bw Sakaja walirushiana maneno makali kwenye mitandao ya kijamii, Bw Owino akilalamikia “huduma duni” katika Kaunti ya Nairobi.

Majibizano yao yalitokana na utafiti uliofanywa na shirika la utafiti la Mizani Africa wiki iliyopita, ambapo Bw Sakaja aliorodheshwa wa mwisho kwenye utendakazi wake, kati ya magavana wote 47 nchini.

“Gavana (Sakaja) amewaangusha wakazi wa Nairobi. Ni vipi unaweza kuorodheshwa wa mwisho kati ya kaunti zote 47? Kazi yako ni kuiba pesa za Kaunti ya Nairobi na kununua nyumba nchini Amerika, London (Uingereza) na Dubai,” akasema Bw Owino.

Akaongeza: “Kando na hilo, anaongeza ushuru anaowatoza wakazi wa Nairobi. Kwa sasa, hata maiti wanatozwa ushuru. Nairobi imeisha. Imetakaa kuwork (akirejelea kauli ya kampeni ya Bw Sakaja: ‘Lazima Iwork’).”

Hata hivyo, Bw Sakaja alimjibu Bw Owino, akisema Nairobi imepata mafanikio makubwa chini ya uongozi wake.

“Huwa ninacheka ninapoona kauli kama hizi. Nairobi imekusanya kiwango kikubwa zaidi cha mapato kwa muda wa miaka mitano iliyopita. Tumefanikiwa kuwalipa Watu wa Kujitolea Kuihudumua Jamii (CHVs) 7,640 kila mwezi kuanzia Agosti mwaka uliopita, tukajenga kituo cha kwanza cha wagonjwa mahututi (ICU), kituo cha pili cha maradhi ya figo, tumejenga majiko kumi kuwalisha watoto zaidi ya 250,000….” akaeleza Bw Sakaja, akirejelea mafanikio aliyopata kwa muda wa mwaka mmoja aliohudumu kama gavana.

Bw Sakaja aliungwa mkono na diwani Robert Alai (Kileleshwa), aliyesema kuwa ni mapema sana kuanza kutathmini utendakazi wake.

“Gavana Sakaja alianza kutumia bajeti yake baada ya Juni, kwani tangu alipoapishwa kuchukua uongozi, amekuwa akitumia bajeti ya Halmashauri ya Kusimamia Jiji (NMS). Hivyo, si haki kutathmini utendakazi wake kwa sasa. Mpeeni muda,” akasema Bw Alai.

Majibizano ya viongozi hao yanajiri muda mfupi tu, baada ya Bw Kuria kumkabili Bw Gachagua, kwa kumkosoa kuhusiana na matamshi yake kwamba Wakenya wanafaa kuchimba visima vya mafuta kutokana na bei ghali ya bidhaa hiyo.

Wadadisi wanataja majibizano hayo kama ishara ya kampeni za mapema ielekeapo 2027.

“Huenda tukaendelea kuona majibizano kama haya, kwani viongozi wengi huanza kuwakosoa wenzao wanaoshikilia nafasi wanazolenga kuwania, ili kuonekana kama watetezi wa raia,” asema mdadisi wa siasa Kipkorir Mutai.

Kwenye majukwaa kadhaa, Bw Owino ameeleza wazi kuwa nia yake ni kuwa rais wa Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Nina mpenzi wa dhati ila napenda kuonjaonja nje

Eneobunge lisilo na hata inchi moja ya lami tangu uhuru

T L