• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Everton wadidimiza matumaini ya Man-United kutwaa taji la EPL

Everton wadidimiza matumaini ya Man-United kutwaa taji la EPL

Na MASHIRIKA

UWEZO wa Manchester United kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu chini ya mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer umetiliwa shaka na mashabiki baada ya kikosi hicho kuambulia sare ya 3-3 dhidi ya Everton mnamo Jumamosi usiku ugani Old Trafford.

Ilikuwa mara ya nne kwa Man-United kuongoza mechi ya ligi katika uwanja wao wa nyumbani kwa angalau mabao mawili kabla ya kuzidiwa ujanja na wageni wao kutokana na utepetevu.

Everton waliwahi kutoka nyuma kwa mabao mawili na kulazimishia Man-United sare ya 4-4 katika michuano ya mikondo miwili ya EPL mnamo Aprili 2012.

Kufikia sasa, Man-United wamefungwa jumla ya magoli 18 kutokana na mechi 12 za nyumbani. Kikosi hicho kilifungwa mabao 17 pekee kutokana na mechi zote 19 walizochezea ugani Old Trafford katika kampeni za msimu wa 2019-20.

Wakicheza dhidi ya Everton mnamo Jumamosi, Man-United walifungua ukurasa wa mabao kupitia Edinson Cavani katika dakika ya 24 kabla ya Bruno Fernandes kuongeza la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Abdoulaye Doucoure na James Rodriguez walisawazishia Everton mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla ya Scott McTominay kuwarejesha Man-United uongozini katika dakika ya 70. Dominic Calvert-Lewin ndiye aliyefanya mambo kuwa 3-3 mwishoni mwa kipindi cha pili na kuhakikisha kwamba Everton ya kocha Carlo Ancelotti inaondoka ugenini na pointi moja iliyowakweza hadi nafasi ya sita jedwalini kwa pointi 37.

Calvert-Lewin amefunga katika mechi tatu zilizopita za EPL kwa mara ya kwanza tangu Oktoba. Sasa anajivunia mabao 13 sawa na Fernandes ambaye pia ni mgombezi halisi wa taji la mfungaji bora katika soka ya Uingereza msimu huu. Hadi alipowaongoza Liverpool kuvaana jana na Manchester City ugani Anfield, nyota Mohamed Salah alikuwa akiongoza orodha ya wafungaji bora wa EPL kwa mabao 15.

Rodriguez aliyesajiliwa kutoka Real Madrid mwanzoni mwa msimu huu, kwa sasa amehusika moja kwa moja katika jumla ya mabao 12 ya Everton na goli dhidi ya Man-United lilikuwa lake la kwanza ugenini katika EPL muhula huu.

Sare dhidi ya Everton iliwasaza Man-United katika nafasi ya pili kwa alama 45 kutokana na mechi 22. Kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer sasa kina presha ya kupitwa na Leicester City na mabingwa watetezi Liverpool wanaofunga mduara wa nne-bora.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kupepetana na West Ham United kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA mnamo Februari 9 ugani Old Trafford kabla ya kuwaendea West Bromwich Albion kwa gozi la EPL mnamo Februari 14.

Kwa upande wao, Everton watakuwa wenyeji wa Tottenham Hotspur kwa minajili ya mchuano wa Kombe la FA mnamo Februari 10 kabla ya kuwaalika Fulham uwanjani Goodison Park kwa pambano la EPL siku nne baadaye.

“Yasikitisha kwamba kikosi kilipoteza alama nyingine muhimu siku chache baada ya kuwaponda Southampton 9-0 ligini,” akatanguliza mwanasoka wa zamani wa Man-United, Paul Scholes.

Kwa mujibu wa jagina huyo wa soka nchini Ungereza, mashabiki wa Man-United wana kila sababu ya kuingiwa na hofu ya kutoshinda taji la EPL muhula huu.

“Ingawa Man-United wanashikilia nafasi nzuri jedwalini, hawachezi kama kikosi chenye kiu ya kutwaa ufalme. Walishindwa kuchuma nafuu kutokana na masihara ya Everton na walishindwa pia kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani licha ya kujivunia uongozi wa mabao mawili katika kipindi cha kwanza. Wanasoka wa Man-United walikosa kujiamini kabisa,” akaongeza Scholes.

MATOKEO YA EPL (Februari 6):

Aston Villa 1-0 Arsenal

Burnley 1-1 Brighton

Newcastle 3-2 Southampton

Fulham 0-0 West Ham Utd

Man-United 3-3 Everton

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ronaldo aongoza Juventus kupepeta Roma

Mipango mikubwa ya rais wa ngumi duniani anayo kwa Kenya