• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Mipango mikubwa ya rais wa ngumi duniani anayo kwa Kenya

Mipango mikubwa ya rais wa ngumi duniani anayo kwa Kenya

Na GEOFFREY ANENE

RAIS wa Shirikisho la Ndondi zisizo za malipo duniani (AIBA) Umar Kremlev ameotoa orodha ya zawadi anapanga kupatia Kenya na Bara Afrika kwa jumla baada ya kuwasili jijini Nairobi mnamno Jumamosi.

Raia huyo wa Urusi, ambaye ni rais wa kwanza kabisa wa AIBA kuzuru Afrika tangu shirikisho hilo lianzishwe mwaka 1946, atasaidia Shirikisho la Ndondi zisizo za malipo Kenya (BFK) kuwa na ukumbi wake katika uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani.

Ukumbi huo utakuwa sehemu ya kufanyia mazoezi itakayowekwa vifaa vya kisasa vya mchezo huo wa ngumi.

“Hatutawapa vifaa tu, bali pia baadhi ya makocha wazuri watakaosaidia BFK kutafuta talanta na kuzifinyanga kutoka umri mdogo mbali na kuimarisha ukufunzi,” alieleza Kremlev, ambaye aliandamana na rais wa Shirikisho la Ndondi zisizo za malipo Afrika (AFBC) Mohamed Moustahsane.

“Tutakuwa na mfumo mzuri wa kifedha utakaoshughulikia kutekelezwa kwa mipango hiyo ili kuhakikisha mchezo wa masumbwi unakuwa nambari moja nchini Kenya,” alisema Kremlev katika hoteli Kempinski.

Isitoshe, Kremlev alifichua kuwa Kenya itakuwa mwenyeji wa mashindano ya kwanza ya kimataifa ya Afrika yatakayotumiwa kuleta pamoja mabondia.

Kremlev, ambaye alichaguliwa Desemba 2020, alikuwa akizungumza baada ya kuwa na kikao na rais wa BFK Anthony “Jamal” Otieno, Katibu katika Wizara ya Michezo Joe Okudo na naibu rais wa kwanza wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) Shadrack Maluki.

Alishukuru uongozi wa BFK kwa kuweka mikakati itakayosaidia kuinua ndondi akisema kuwa Kenya ina historia ndefu ya mchezo huo ikiwemo kutoa mmoja wa mabondia wawili kutoka Afrika kuwahi kushinda medali ya dhahabu kwenye Olimpiki, Robert Wangila.

“Kenya ina mabingwa kadhaa wa dunia katika ndondi, lakini nimekuja hapa kusaidia kuinua mchezo huu kufika kiwango cha juu nchini Kenya na Afrika kwa jumla. Ni mapenzi ya Mungu kuwa niwe rais wa kwanza wa AIBA kuzuru Afrika, hasa Kenya,” alisema.

Mmoroko Moustahsane, ambaye alitumikia AIBA kama kaimu rais baada ya Mwamerika Tom Virgets kuondolewa mamlakani kati ya Machi 2019 na wakati uchaguzi uliandaliwa Desemba 2020, aliahidi kusaidia Kremlev kutimiza mipango yake mikubwa na kuimarisha mchezo wa masumbwi katika miezi michache ijayo.

“Kenya inafahamika kwa michezo na tutahakikisha inapata sifa iliyopotea. AIBA itakuwa tena shirikisho linaloenziwa,” alisema Moustahsane.

Kremlev atakuwa na kikao na mataifa wanachama wa shirikisho hilo kutoka Afrika kitakachoendeshwa kupitia kwa mtandao kutoka jijini Nairobi, Jumapili.

  • Tags

You can share this post!

Everton wadidimiza matumaini ya Man-United kutwaa taji la...

JAMVI: Sonko alivyojipalia makaa mwenyewe