• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Familia ya Masten Wanjala yamkana, mwili wasalia mochari

Familia ya Masten Wanjala yamkana, mwili wasalia mochari

Na BRIAN OJAMAA

MWILI wa Masten Wanjala, mwanamume aliyekamatwa kwa mauaji ya watoto, bado uko katika mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Bungoma, majuma mawili baada ya kuuawa na umati wenye ghadhabu.

Hali hiyo imejiri baada ya familia na ukoo wake kukataa kumkubali kama mmoja wao. Familia hiyo imekataa kuuchukua mwili wake ili kuuzika.

Wanjala aliuawa na wakazi wenye ghadhabu katika kijiji cha Mukhweya, eneobunge la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma, umbali wa kilomita moja kutoka makazi ya wazazi wake.

Familia pia ilikataa kushiriki kwenye zoezi la kuufanyia upasuaji mwili wake ikiongozwa na babake, Bw Robert Watila.

Upasuaji huo ulifanywa Jumatano iliyopita na maafisa kutoka Idara ya Kupeleleza Uhalifu (DCI), wakiongozwa na Bw Martin Nyuguto katika mochari hiyo.

Mmoja wa jamaa zake ambaye hakutaka kutajwa, alisema familia bado ina maswali jinsi mwanao alifaulu kutoroka seli na kusafiri hadi kwao.

“Tunashuku polisi walihusika kwenye mauaji ya ndugu yetu. Sababu ni kwamba mara ya mwisho tuliposikia habari kumhusu, alikuwa analindwa vikali na polisi. Kuna maswali kuhusu namna alivyofanikiwa kutoroka na kusafiri hadi nyumbani hadi akauawa,” akasema.

Aliongeza familia hiyo inatathmini kuishtaki serikali kutokana na kifo cha mwanao.

Naibu Chifu wa Kata Ndogo ya Mukhweya, Bw Abiud Musungu, aliiambia Taifa Leo kwamba maafisa wa serikali wamejaribu kuiomba familia na ukoo wa Bakitwika Kitanga kuchukua matokeo ya DNA ili kumzika mwanao lakini zimetakaa.

Alisema familia hiyo imeomba muda zaidi kufikiri na kushauriana.

You can share this post!

Kiraitu atakiwa kulipa Sh274m kabla ya kukabidhiwa chama

Shinikizo Uingereza ichunguze mwanajeshi anayehusishwa na...

T L