• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Familia yahofia ‘pepo wa mauti’ huwafyeka watoto wa kiume Jumapili

Familia yahofia ‘pepo wa mauti’ huwafyeka watoto wa kiume Jumapili

NA KALUME KAZUNGU

FAMILIA katika kijiji cha Kiangwe, Kaunti ya Lamu, yapanga kufanya tambiko la kitamaduni baada ya watoto wao watatu wa kiume kufariki miaka tofauti katika hali za kushangaza, wote wakifa Jumapili.

Katika Jumapili ya Aprili 16, 2017, Yusuf Hussein Shizo, 10, alikufa maji.

Mnamo Septemba 30, 2018, Issa Hussein Shizo, 25, alidungwa kisu katika ugomvi wa miraa na akafa; naye Omar Hussein Shizo, 18, akapatikana ameuawa mnamo Aprili 9, 2023, ikidaiwa alipigwa na polisi.

Mbali na watatu hao wote kufariki katika hali zinazohusishwa na mauaji Jumapili, vifo vya Yusuf na Omar pia vilitokea katika kipindi cha Pasaka.

Mama yao, Bi Mariam Mohamed Hilesi, amejawa wasiwasi kuhusu matukio haya. Alijaliwa watoto sita, ambapo wavulana walikuwa wanne na wasichana wawili.

Sasa amesalia na mvulana mmoja pekee, na binti zake wawili.

Kifo cha Yusuf, ambaye alikuwa kitinda mimba, kilitokea alipokuwa akiogelea na watoto wenzake kwenye fuo za Bahari Hindi karibu na kijiji cha Kiangwe mnamo 2017.

Issa naye, ambaye alikuwa kifungua mimba, aliuawa mwaka wa 2018 ugomvi ulipotokea kati yake na mzee wa umri wa miaka 68 wakati huo, Omar Lola Hussein, walipokuwa wakitafuna miraa kijijini. Lola alishtakiwa na kwa sasa bado anatumikia kifungo gerezani.

Kisa cha hivi punde zaidi ambacho kimetia msumari moto kwenye kidonda cha familia hiyo ni kile cha Jumapili, ambapo maiti ya mwana wao wa tano, Omar ilipatikana karibu na kambi ya polisi wa kushika doria za mpaka wa Kenya na Somalia (BPU) kijijini Kiangwe.

Ilidaiwa kuwa, kabla apatikane akiwa ameaga dunia, Omar alikuwa amepelekwa na chifu wa eneo hilo kwa kambi ya polisi baada ya kutuhumiwa aliiba kilo tano za unga wa mahindi. Unga huo ulikuwa sehemu ya vyakula vya msaada vya Ramadhani vilivyokuwa vikisambazwa na wahisani kwa wanakijiji. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Bw William Samoei, alisema kisa hicho kinachunguzwa.

“Nina wasiwasi. Warithi wa familia wote wanafariki. Nimepoteza vijana watatu kufikia sasa katika hali ya kushangaza. Naomba usaidizi nipate haki kwa wanangu waliouawa,” akasema Bi Hilesi.

Bi Hilesi anasisitiza haja ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kuingilia kati ili kusaidia familia yake kupata haki kwa vijana wawili waliouawa.

Zaidi ya hayo, familia hiyo ilisema kuwa, inajiandaa kufanya tambiko ili kufukuza mkosi wa mauti ambao umekuwa ukiiandama na kulenga watoto wa kiume.

Bw Hussein Shizo Gorke, ambaye ndiye baba katika familia hiyo, alisema anaamini tambiko litakalofanywa na jamii yao ya Waboni pia litasaidia kuhakikisha haki inatendeka kwa vijana wawili waliouawa.

“Huku tukiendelea kufumbua kitendawili cha mauti ya vijana wetu, pia tumeona haja ya kufanya tambiko ili kufurusha hili pepo la mauti linaloandama familia yangu,” akasema Bw Gorke.

Akizungumzia kisa cha Jumapili, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Bw Samoei aliomba jamii kuwa tulivu ili kutoa nafasi ya uchunguzi kwa njia ya haki.

  • Tags

You can share this post!

Manchester City guu moja ndani ya nusu-fainali UEFA

Familia yataka ukweli kuhusu kifo cha mtoto,15

T L