• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Gachagua: Ninaweza kufundisha Kiingereza katika Shule ya Upili

Gachagua: Ninaweza kufundisha Kiingereza katika Shule ya Upili

NA SAMMY WAWERU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesema anajiamini kufunza Somo la Kiingereza na Fasihi (Literature) katika shule ya upili, kutokana na uweledi wake kwenye lugha hiyo.

Bw Gachagua alifichua kwamba alipata alama bora zaidi (Distinction One) katika Fasihi ya Kiingereza.

Katika video inayosambaa mitandaoni, Naibu wa Rais akiwa na wahitimu wa Shule ya Upili ya Kianyaga, alisema yuko tayari kurejea darasani na kunoa wanafunzi makali ya Kizungu.

Alisimulia kumbukumbu zake baada ya kuhitimu Kidato cha Nne, na kabla kujiunga na Chuo Kikuu.

Kinyume na muda wa sasa waliofuzu Mtihani wa Kitaifa Kidato cha Nne (KCSE) kujiunga na chuo kikuu, miaka ya awali wanafunzi walikawia hadi miaka miwili.

Anasema, kwa kipindi cha muda wa mwaka mmoja na nusu alifunza Kiingereza na Fasihi katika shule moja ya upili Machakos.

“Nilifunza kama mwalimu asiye na mafunzo…Kati ya Kidato cha sita na chuo kikuu, kulikuwa na tatizo; Wanafunzi walikuwa wakisubiri hadi miaka miwili kabla kuingia chuo kikuu,” Naibu Rais alifichua.

Bw Gachagua ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Upili ya Kianyaga, iliyoko katika Kaunti ya Kirinyaga.

Alikumbuka, “Niliondoka Kianyaga mwishoni mwa mwaka wa 1983 na kisha kujiunga na chuo kikuu Oktoba 1985. Kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu, nilifundisha katika shule ya upili huko Machakos.”

“Wakati huo, nilifundisha Kiingereza na Fasihi ya Kiingereza. Nilifanya bora zaidi katika Fasihi. Siku moja, nitarudi na kusomesha,” Naibu Rais alisema, huku akizua ucheshi.

Gachagua pia alifichua kuwa wakati wa kufundisha kwake Machakos, alizindua mchezo wa voliboli shuleni, urithi ambao unaendelea kufanikiwa.

Alisema kwamba yeye ni hodari katika voliboli.

Gachagua anajulikana kwa kutoa kauli zenye mzaha mara kwa mara, mara nyingi akiwa anakumbuka safari yake ya maisha na wakati akihudumu kama D.O.

Katika mojawapo ya tani zake, alikiri wazi kwamba alikuwa mateka wa unywaji pombe kupita kiasi.

Hata hivyo, baadaye aliacha tabia ya kunywa vileo.

Chini ya serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto, Gachagua amepewa jukumu la kupambana na kero ya pombe haramu na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na mihadarati.

Alianza operesheni hiyo Mlima Kenya, eneo analotoka, na ameahidi kwamba mapambano hayo yataelekezwa maeneo mengine nchini.

Mkewe, Bi Dorcas Gachagua ni pasta.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume Murang’a ajitoa uhai kwa kukosa Sh30, 000...

Polo alia kama senge lojing’i Murang’a baada ya...

T L