• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Gavana Mutula achemkia wanaobwabwaja siri za serikali yake

Gavana Mutula achemkia wanaobwabwaja siri za serikali yake

NA PIUS MAUNDU

GAVANA Mutula Kilonzo Junior wa Makueni, jana alitoa onyo kali kwa wafanyakazi wa serikali hiyo ambao wamekuwa wakiweka stakabadhi muhimu za serikali kwenye mitandao ya kijamii.

Akiwahutubia maafisa wakuu wa kaunti katika hafla fupi kutathmini utendakazi wa serikali yake, Bw Kilonzo alisema uwekaji wa stakabadhi hizo kwenye mitandao ya kijamii ni kosa kubwa.

Gavana aliiagiza Bodi ya Kuajiri Wafanyakazi Kaunti kuwachukulia hatua wafanyakazi wanaoweka mitandaoni stakabadhi rasmi za serikali.

“Kuna maafisa wanaodhani ni vizuri kuweka siri za serikali kwenye mitandao ya kijamii. Tuna shida. Ni suala lenye uzito sana. Unaweza kufanya hivyo ukifikiri unamharibia sifa mtu mwingine, ila unajiharibia wewe mwenyewe. Kwa sasa nimenyamaza, ila nitakabiliana na suala hili wakati ufaao,” akasema.

Onyo la gavana huyo linajiri huku serikali yake ikiendelea kuelekezewa lawama kutokana na utendakazi wake.

Kwa wiki mbili zilizopita, kumekuwa na mijadala mikali katika mitandao ya kijamii kutokana na malalamishi hayo.

Mijadala hiyo iliibuliwa na stakabadhi kadhaa za serikali zilozowekwa mitandaoni.

Stakabadhi hizo, baadhi zilizo mikononi mwa Taifa Leo, zinaangazia taratibu za utoaji tenda katika Idara ya Afya na ushauri wa kiufundi uliotolewa kuhusu mpango wa kuwapandisha ngazi baadhi ya maafisa wakuu katika kaunti.

Wiki iliyopita, makachero mjini Wote waliwahoji maafisa watatu wa ngazi za juu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Makueni, kuhusu ikiwa walihusika kwa vyovyote vile kuweka mitandaoni stakabadhi zinazoonyesha kuwa Bw Kilonzo haridhishwi na utendakazi wa serikali hiyo.

Hofu hizo ndizo zinazoelezwa kumfanya Bw Kilonzo kumwagiza Waziri wa Afya, Paul Musila, kulainisha utendakazi wa idara hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Mshtakiwa wa ulaghai wa mashamba anyimwa dhamana

Madiwani wadai wameona makosa 12 ya kuwawezesha...

T L