• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Madiwani wadai wameona makosa 12 ya kuwawezesha kumng’atua gavana Nyaribo

Madiwani wadai wameona makosa 12 ya kuwawezesha kumng’atua gavana Nyaribo

NA WYCLIFFE NYABERI

MADIWANI wa Nyamira wameorodhesha sababu 12 za kutaka kumng’atua Gavana Amos Nyaribo.

Miongoni mwa sababu hizo ni madai kuwa gavana huyo amekuwa akikiuka katiba na kwamba amekuwa akiajiri wafanyakazi wa kaunti kwa kutofuata sheria.

Pia wamemnyooshea Nyaribo kidole cha lawama kwa kile wanasema amekuwa akipuuza maagizo ya mahakama, kutotuma pesa za makato ya wafanyakazi wa umma, kuwaajiri kazi jamaa wake wa karibu miongoni mwa sababu nyingine.

Sababu hizo zimewekwa bayana Jumanne wakati hoja ya kung’atuliwa kwake imewasilishwa bungeni na diwani wa Esise Josiah Mang’era.

Ni MCAs 27 waliokuwa bungeni wakati wa kuwasilishwa kwa hoja hiyo.

Usiku wa kuamkia Jumanne, kinyesi cha binadamu na mawe lori nzima vilipatikana vimemwagwa nje ya lango la kuingia kwenye bunge la kaunti hiyo.

Vizuizi hivyo vililetwa usiku wa manane na watu wasiojulikana kama njia mojawapo ya kutatiza kuwasilishwa kwa mswada huo.

Maafisa wa polisi wakishirikiana na wale wa kutekeleza amri za kaunti walishika doria kwenye lango kuu wakikagua kwa makini kila aliyekuwa akiingia.

Mzozo kati ya madiwani na gavana Nyaribo ulitokota pale kiongozi huyo wa chama cha United Progressive Alliance (UPA) alimfuta kazi waziri wake wa Afya Timothy Ombati.

Bw Nyaribo alisema Bw Ombati alikuwa amehusika kwa ufujaji wa pesa zilizohitajika kwenye ununuzi wa dawa hospitalini.

Alidai waziri huyo alimhadaa kuzindua maboksi tupu ambayo hayakuwa na dawa ndani.

Hata hivyo, Bw Ombati alikana madai hayo, baadhi ya madiwani wakimtetea kwa kusema alikuwa mwathiriwa tu wa sakata kubwa ya ufisadi inayokumba serikali ya Nyamira.

Jana (Jumatatu), Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Silvanus Osoro alikutana na madiwani hao na kuwasihi watatue mzozo wao kiustaarabu lakini wakamweleza kwamba hawatalegeza kamba.

Pia gavana Nyaribo amekuwa akiwasihi MCAs hao wajadiliane kuondoa uasi baina yao lakini mikakati yake haijafua dafu.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Mutula achemkia wanaobwabwaja siri za serikali yake

Kate Actress sasa atishia kushtaki TUKO kwa kumchafulia jina

T L