• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Genge laibuka upya nakujeruhi watu 7 mtaani

Genge laibuka upya nakujeruhi watu 7 mtaani

Na WACHIRA MWANGI

WATU zaidi ya saba walijeruhiwa baada ya genge la wahalifu wenye visu na panga kushambulia wakazi mtaani Bashir, katika Kaunti ya Mombasa.

Tukio hilo la usiku wa kuamkia jana limewaacha wakazi wa mtaa huo na viungani mwake kuwa na wasiwasi kwamba huenda wahalifu hao wakarudi tena kuwavamia.

Mkuu wa polisi eneo la Nyali, Bw Daniel Mumasaba akithibitisha shambulio hilo, alisema msako umeanzishwa kuwanasa majambazi hao wanaoshukiwa kuwa wanachama wa genge la Wakali Kwanza ambalo limekuwa likiwasumbua wakazi katika maeneo ya Kisauni.

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo alisema washukiwa wawili walikamatwa na wako katika kituo cha polisi cha Kadzandani wakisubiri kufikishwa mahakamani kufunguliwa mashtaka ya wizi na kusababisha vurumai.

‘Tulipata habari kutoka kwa waendeshaji bodaboda kwamba kulikuwa na kundi la vijana ambao walionekana ndani ya shule ya msingi ya Bashir, wanaoshukiwa kuwa na silaha hatari,’ Bw Kitiyo alisema.

Aliongeza kuwa operesheni ya polisi kutoka vitengo mbalimbali ilisaidia sana katika kuhakikisha washukiwa hao wamekabiliwa vilivyo kabla wasababishe maafa.

Waliokamatwa katika operesheni hiyo ni Bw Brian Teka na Bashora Yusuf, wenye umri wa miaka 17. Polisi walisema washukiwa hao walipatikana na mapanga ambayo walitumia katika uvamizi huo.

Taarifa za polisi zinaonyesha kuwa wawili hao awali walimnyang’anya Bw Kennedy Khisa, mkazi wa Nguu Tatu, kiwango cha pesa kisichojulikana kabla ya kumkata kwa panga kwenye paji la uso.

Wawili hao pia wanashukiwa kumkata Bw Peter Kigany kwenye paji la uso.Bomu la petroli lililotengenezwa nyumbani lilipatikana katika eno la tukio.

Bw Leonard Kai ambaye alipata jeraha mkononi alisema kuwa vijana hao walitekeleza uvamizi huo baada ya kutoka kwenye sala ya jioni ya Waislamu mara tu baada ya Iftar.

Kigany aliumia kwenye mkono wake wa kushoto alipojaribu kujikinga ili asikatwe kwenye kichwa. ‘Vijana hao walikuwa zaidi ya 30. Walianza kukata watu kwa panga kiholela. Walianzia eneo la Bashir, ”Bw Kai alisema.

Waendesha bodaboda walioshuhudia kisa hicho walielezea hofu yao huku wakitaka vitengo vya usalama kulifuatilia suala hilo ili kuwahakikishia usalama wanapotafuta riziki yao ya kila siku.

Vijana hao pia walishambulia gari la kusafirisha tuk-tuk na kuharibu baadhi ya mali hizo.Muuzaji wa maji katika hatua ya kumnusuru Bashir alinyang’anywa simu genge hilo la vijana lilipokuwa likikimbia.

Bw Pascal Kahindi alipata jeraha usoni baada ya kupigwa na vijana hao. Bw Daniel Obedi ambaye anafanya kazi ya ulinzi alipata jeraha ya kichwa wakati wa shambulizi hilo.

Bi Salma Salim mkazi wa eneo la Bashir huko Kisauni alilalamikia hali duni ya usalama katika eneo hilo. Amevitaka vitengo vya ulinzi kuwahakikishia wakazi usalama.

You can share this post!

Mwaura apoteza useneta rasmi na kiti kutangazwa wazi

Buffon kuagana rasmi na Juventus mwishoni mwa msimu huu