• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Hakuna kulipa zaidi kuegesha magari jijini

Hakuna kulipa zaidi kuegesha magari jijini

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu Jumatano ilisitisha hatua ya kaunti ya Nairobi kuongeza ada ya kuegesha magari ya kibinafsi na matatu hadi kesi iliyoshtakiwa na shirika la kitaifa la watumizi wa bidhaa (Cofek) itakaposikizwa na kuamuliwa.

Jaji Antony Mrima alizima hatua ya kaunti ya Nairobi kuongeza ada ya kuegesha magari ya kibinafsi kutoka Sh200 hadi Sh400.

Wenye magari ya matatu walitakiwa walipe ada mpya kati ya Sh8,500 na Sh10,000 kulingana na idadi ya abiria.

Mwaka uliopita kaunti ya Nairobi ilichapisha katika Gazeti rasmi la Serikali kwamba itaongeza ada ya kuegesha magari ya kibinafsi na matatu.

Shirika la Cofek na chama wenye matatu kiliishtaki kaunti na Jaji Aaron Makau akasitishe kutekelezwa kwa ada hizo zilizochapishwa katika Gazeti hilo hadi kesi iliyoshtakiwe isikizwe na kuamuliwa.

Baada ya kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 kesi haikuendelea kwa vile huduma za mahakama zilivurugwa.

Jana Jaji Mrima aliombwa na Bw Henry Kurauka aruhusu agizo la kusitishwa kwa nyongeza iendelee kuibana kaunti ya Nairobi.

Bw Kurauka anayewakilisha Cofek alisema nyongeza hiyo ililenga kuwakandamiza wakazi wa Nairobi aliosema pia wameathiriwa na makali ya ugonjwa wa Covid-19.

Bw Kurauka anayewakilisha Cofek aliomba agizo iliyotolewa mwaka jana ikipiga breki hatua ya kuongeza ada hizo iendelee kutumika kwa vile wakazi wote wa jijini Nairobi wameathirika kiuchumi kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

“Athari za ugonjwa wa Covid-19 zimeathiri pakubwa huduma zote za kiuchumi kwa watu binafsi na wenye magari ya matatu,” Bw Kurauka alimweleza Jaji Mrima wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa maagizo zaidi.

Bw Kurauka alisema wakazi wa jijini Nairobi wameathiriwa pakubwa huku wengi wao hata wakipoteza kazi zao.

Wakili huyo alimsihi Jaji Mrima apige breki hatua hii ya kaunti ya Nairobi ya kuongeza ada hiyo ya kuegesha magari ya kibinafsi na pia matatu.

Jaji huyo alielezwa tangu  ugonjwa wa Corona ulipuke ,magari yote ya matatu yaliagizwa yapunguze idadi ya abiria inayowabeba.

“Mapato ya wenye magari ya matatu yalipungua kabisa kwa vile idadi ya abiria ilipunguzwa kwa nusu,” Jaji Mrima alifahamishwa.

Mahakama ilielezewa na Bw Kurauka wenye magari “waliamriwa wafuate sheria za Wizara ya Afya na mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) za kukinga abiria,” Bw Kurauka alieleza mahakama.

Jaji Mrima aliamuru kesi hiyo isikizwe Aprili 21,2021.

  • Tags

You can share this post!

Askofu ataka serikali ichanje Wakenya wote

Akana kumlaghai mwenzake Sh36m