• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Akana kumlaghai mwenzake Sh36m

Akana kumlaghai mwenzake Sh36m

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA alishtakiwa Jumatano kwa kumlaghai mwenzake Sh36milioni akijifanya angelimuuzia shamba ekari moja katika mtaa wa kifahari wa Karen kaunti ya Nairobi.

Bi Hadija Asif Batt alifikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku.

Alikabiliwa na shtaka kwamba kati ya Septemba 2014 na Desemba 30 2016 akiwa na nia ya kulaghai alipokea kitita cha Sh36m kutoka kwa  Bw Molu Halkano akidai alikuwa na uwezo wa kumuuzia shamba katika mtaa wa kifahari wa Karen kaunti ya Nairobi.

Bi Batt alikana shtaka dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

“Sitatoroka mbali nitatii masharti nitakayopewa na hii mahakama ikiniachilia kwa dhamana,” akarai Bi Batt.

Mshtakiwa alimweleza hakimu kwamba alikuwa ameachiliwa kwa dhamana ya Sh180,000 na polisi uchunguzi ukiendelea.

“Nilishirikiana na wachunguzi katika kesi hii kila wakati. Nilifika katika afisi za uchunguzi wa ulaghai wa mashamba kitengo cha DCI bila kukosa,” alisema Bi Batt.

Mshtakiwa huyo alikamatwa na Polisi mnamo Januari 29 2021 baada ya mlalamishi Bw Halkano kupiga ripoti alifujwa pesa katika ulaghai wa ardhi.

Alimweleza hakimu kuwa alikuwa ameamriwa na polisi ajisalamishe kortini Machi 3,2021 ajibu shtaka.

“Nilifika kortini kama nilivyoagizwa na afisa anayechunguza kesi hii Konstebo Lumwachi,” mshtakiwa alimweleza hakimu huku akisema atatii masharti ya dhamana.

Kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda hakupinga ombi hilo.

Bi Mutuku alimwachilia Bi Batt kwa dhamana ya Sh3milioni pesa tasilimu.

Kesi itatajwa katika muda wa wiki mbili.

  • Tags

You can share this post!

Hakuna kulipa zaidi kuegesha magari jijini

Suluhu azima nyongeza ya ushuru, Wakenya wazidi kuumia