• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Hatima ya watoto 50,000 yaning’inia Serikali ikipanga kufunga makao yanayosimamiwa na watu binafsi

Hatima ya watoto 50,000 yaning’inia Serikali ikipanga kufunga makao yanayosimamiwa na watu binafsi

NA MARY WANGARI

SERIKALI imetangaza mipango ya kufunga taasisi zote za kibinafsi za malezi ya watoto na mayatima katika juhudi za kukabiliana na kero la ulanguzi wa watoto.

Hata hivyo, hatua hiyo inaibua maswali kuhusu hatima ya maelfu ya watoto wanaolelewa na mamia ya vituo vinavyoendeshwa na wahisani wa kibinafsi.

Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii Florence Bore amefichua kuwa serikali inapanga kutekeleza hatua hiyo katika muda wa miaka minane ili kuhakikisha watoto wote hatimaye wanajumuishwa katika jamii.

Aidha, alisema ni taasisi zinazomilikiwa na serikali pekee zitakazoruhusiwa kuendelea kuwapa makazi na malezi watoto waliotelekezwa au kuokolewa.

Waziri alisema haya Jumatatu, Octoba 2, 2023 katika Kituo cha Uokoaji Murang’a, kinachoendeshwa na Jumuiya ya Maslahi ya Watoto Nchini (CWSK) wakati wa ziara yake ya kukagua vituo vya malezi ya watoto.

“Tunajaribu kuzima vituo vyote binafsi vya uokoaji kando na vituo vya kiserikali hususan kwa sababu ya ulanguzi wa watoto. Tunataka kuhakikisha hilo halifanyiki nchini,” alisema Waziri Bore.

Alifafanua kuwa serikali inadhamiria baada ya muda “watoto hawa wajumuishwe kwenye familia katika jamii. Baadhi yao wapangwe ili wakue katika mfumo wa familia na kuwa raia wa taifa hili wanaowajibika na hatimaye tuwarejeshe katika jamii. Kwa wale hawana jamaa tutaendelea kuwapa malezi hadi watakapokua.”

Kulingana na Waziri, kwa sasa kuna watoto karibu 400 katika shule za upili wanaosomeshwa na CWSK.

Kituo cha Uokoaji Murang’a kinachoendeshwa na CWSK, kwa mfano, kina jumla ya watoto132 ambapo 82 wako katika shule za sekondari huku 50 wakiwa na umri kati ya miaka 3 – 10.

“Nimefurahia kazi inayofanywa na CWSK. Tunatoa wito kwa Wakenya wenye nia njema kusaidia Jumuia katika jitihada zake za kulea watoto hawa. Tuna watoto ambao wametupwa, kunajisiwa…kama Wizara, tunataka kuhakikisha watoto wetu hawatelekezwi, kwamba watatunzwa vyema.”

Kufikia Novemba 2022, kulikuwa na watoto kati ya 45,000 – 50,000 katika vituo vya kibinafsi takriban 855 huku wengine wakipata afueni katika taasisi za kiserikali, kulingana na takwimu kutoka Idara ya Ulinzi wa Jamii.

Tangazo hili limejiri wiki moja baada ya Waziri Bore kueleza Seneti kuwa Wizara yake imeanza kuandikisha kundi jipya la watu wanaojumuisha mayatima, wazee na walemavu watakaokuwa wakipokea Sh2,000 kila mwezi kupitia mpango wa serikali.

“Tunaandikisha kundi jipya la watu 500,000 wanaojumuisha wazee, walemavu na mayatima. Tuna nafasi nyingine 190,000 ambazo zimeachwa wazi kutokana na sababu za kimaumbile,” alifafanua Waziri.

  • Tags

You can share this post!

Hofu yatanda chokoraa wakianza kujaa ushago

Mzozo wa uongozi unavyotikisa kanisa la Kianglikana...

T L