• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 7:55 AM
Historia yawafaa Ruto, Raila 50:50

Historia yawafaa Ruto, Raila 50:50

Na CHARLES WASONGA

HISTORIA ya kinyanga’anyiro cha urais nchini inaonyesha ushindi wa Agosti 9 unaweza kwenda upande wowote kati ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto.

Kwa kigezo cha majaribio ambayo mwaniaji amefanya kuingia Ikulu, historia inamfaa Bw Odinga ambaye amejaribu bahati mara nne bila mafanikio.

Lakini kwa kigezo cha Bw Odinga kuonekana kuwa mradi wa rais anayeondoka, historia inaonekana kumpendelea Dkt Ruto.

Kwa upande wa Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka, historia inawafungia njia ya Ikulu kwani kinyang’anyiro cha urais hapa Kenya kimekuwa ni kati ya vigogo wawili wakuu ambao mwaka huu ni Bw Odinga na Dkt Ruto.

Hii ni licha ya wawili hao kuwania awali.Katika kigezo cha majaribio tangu 2002, hakuna mwaniaji aliyeshinda kiti hicho katika jaribio la kwanza.

Rais mstaafu Mwai Kibaki aliingia Ikulu katika jaribio lake la tatu mnamo 2002.

Awali aliwania urais mnamo 1992 na kuibuka katika nafasi ya tatu na 1997 aliposhika nafasi ya pili nyuma ya Daniel Moi.

Rais Uhuru Kenyatta naye alishinda urais katika jaribio lake la pili. Mara ya kwanza alipigania kiti hicho akiwa mradi wa Bw Moi mnamo 2002 ambapo aliangushwa na Mzee Kibaki.

MWANASIASA MZOEFU

Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa wanasema hali ya sasa ni tofauti na ilivyokuwa mnamo 2002 kwani Bw Kenyatta alikuwa limbukeni wa siasa aliyesukumwa na Bw Moi kuingia kwenye siasa na hata kuwania urais, wakati huo akiwa na miaka 41.

Tofauti na Bw Kenyatta wakati huo, Dkt Ruto akiwa na miaka 55 ni mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa na anayejulikana kote nchini.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, kwa kuzingatia kigezo cha kujaribu bahati ya urais mara nyingi, historia inamfaa Bw Odinga.

“Ni kweli kwamba tangu utawala wa Kanu kuondolewa mamlakani 2002, washindi wa urais wamekuwa wagombeaji ambao wamejaribu angalau mara moja tukirejelea Kibaki na Uhuru. Kwa hivyo, pamoja na sababu nyinginezo, nyota ya Raila inang’aa zaidi mwaka huu ikilinganishwa na Dkt Ruto anayejaribu kwa mara ya kwanza,” anasema Bw Andati ambaye pia ni mshauri wa masuala ya uongozi.

KUWANIA URAIS MARA YA TANO

Bw Odinga anawania urais kwa mara ya tano katika uchaguzi wa mwaka huu, baada ya kufeli mara nne katika chaguzi za 1997, 2007, 2013 na 2017.

Katika uchaguzi mkuu wa 1997 Bw Odinga alishikilia nafasi ya tatu alipowania kwa tiketi ya chama cha National Development Party (NDP) alipopata kura 667,886 pekee.

Katika uchaguzi mkuu wa 2007 alikuwa wa pili kwa kupata kura 4.35 milioni nyuma ya Bw Kibaki aliyeshinda kwa kuzoa kura 4.58 milioni, tofauti ya kura 231,000 pekee.

Katika changuzi za 2013 na 2017, Bw Odinga alishindwa na Rais Kenyatta, alipopata kura 6.17 milioni na 6.3 milioni, mtawalia.

Lakini Bw Dismus Mokua anasema hali ya kisiasa nchini katika uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na wa chaguzi zilizopita.

“Ushindi wa Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, hautachangiwa zaidi na historia ya matokeo ya uchaguzi wa urais lakini kutokana na kiwango ambapo Rais Kenyatta ataweza kushawishi eneo la Mlima Kenya kumpigia kura. Vile vile, ushindi wake utategemea pakubwa ikiwa Bw Odinga ataweza kupata uungwaji mkono kutoka kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka au la,” anasema mchanganuzi huyo wa masuala ya siasa.

Kulingana na Bw Mokua, Bw Odinga atakuwa na kibarua kikubwa endapo wakazi wengi wa Mlima Kenya, yenye zaidi ya kura milioni sita, watasalia kumuunga mkono Dkt Ruto na eneo la Ukambani lenye karibu kura 2 milioni lisalie na Bw Musyoka.

Lakini kwa kuzingatia historia ya mwaniaji kuwa mradi wa rais anayeondoka, Dkt Ruto atakuwa na nafasi bora.Mnamo 2002 Bw Moi alipomfanya Bw Kenyatta kuwa mradi wake, Wakenya waliasi kwa kumchagua Mzee Kibaki kwa idadi kubwa ya kura.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Bw Odinga amejitokeza kuwa mradi wa Rais Kenyatta.

“Raila ni mradi wa Uhuru na atafeli jinsi Uhuru mwenyewe alivyoshindwa na Kibaki alipokuwa mradi wa Rais wa Moi,” anaeleza Seneta wa Nandi, Samsom Cherargei.

Mwingine aliyetangaza kuwania urais ni Reuben Kigame ambaye historia inampa nafasi finyu kupata kura nyingi.

You can share this post!

Zai pits ni muhimu kwa wakulima katika maeneo kame

UDA yaondoa ada ya uteuzi kwa wanaoishi na ulemavu

T L