• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
UDA yaondoa ada ya uteuzi kwa wanaoishi na ulemavu

UDA yaondoa ada ya uteuzi kwa wanaoishi na ulemavu

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kimewaondolea ada za uteuzi Wakenya wanaoishi na ulemavu (PLWD) ambao wanataka kuwania viti vyote sita katika uchaguzi mkuu Agosti 9, 2022.

Chama hicho pia kimepunguza ada hizo kwa kiwango cha asilimia 50 kwa vijana na akina mama ambao wangetaka kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi huo wa Agosti 9.

Hii ni kulingana na chapisho la chama hicho kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto katika magazeti Jumatano, Februari 2, 2022 na mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya UDA Anthony Mwaura.

Kulingana na chapisho hilo, watu wanaosaka tiketi ya UDA kuwania urais watahitajika kulipa Sh1 milioni kama ada ya uteuzi. Hii ina maana kuwa wanawake wanaotaka tiketi hiyo watalipa Sh500,000.

Hii ina maana kuwa wanaume wanaotaka udhamini wa UDA kuwania ugavana na useneta watahitajika kulipa Sh500,000 huku wanawake wakilipa Sh250,000 kila mmoja.

Wawaniaji wa nyadhifa za Ubunge na Mbunge Mwakilishi watahitajika kulipa Sh250,000 huku wale wanaowania udiwani wakitakiwa kulipa ada ya uteuzi huku wanawake wakilipa nusu ya kiasi hicho.

Wanaume ambao watataka kuwania udiwani kwa tiketi ya UDA watatakiwa kulipa Sh50,000 huku wanawake wakilipa Sh25,000.

Hata hivyo, Wakenya wamewasilisha malalamishi mitandaoni kuhusu ada hizo wakisema ni za juu zaidi kwa Wakenya wenye mapato ya chini, maarufu kama ‘mahasla’.

“UDA ni chama cha mahasla lakini ada ya uteuzi wake ni juu zaidi ikizingatiwa wakati huu Wakenya wanapitia hali ngumu ya kimaisha kutokana na kudorora kwa uchumi,” akasema Mkenya aliyejitambua kwa jina moja la, Roy.

You can share this post!

Historia yawafaa Ruto, Raila 50:50

Pesa zipo katika mimea ya mafuta, asema mmiliki wa kiwanda

T L