• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 4:26 PM
Zai pits ni muhimu kwa wakulima katika maeneo kame

Zai pits ni muhimu kwa wakulima katika maeneo kame

Na SAMMY WAWERU

MOJAWAPO ya mifumo ambayo Urbanus Kamuti amekumbatia, ni matumizi ya Zai pits.

Anaendeleza shughuli za kilimo katika kipande cha ardhi katika eneo kame, kaunti ndogo ya Mwala, Machakos, eneo ambalo mvua kushuhudiwa ni mara chache mno kwa mwaka.

Hukuza mboga za kienyeji kama vile mnavu, mchicha (terere), kunde, sukumawiki na pia spinachi.

Katika shamba hilo la Urbanus, amepanda michungwa inayozaa machungwa aina ya Pixies na hata ile ya machungwa ya kawaida, na vile vile matikitimaji.

Yeye pia hukuza nyanya, mahindi na maharagwe.

Kulingana na mkulima huyu wa haiba yake, alikumbatia mfumo wa Zai pits baada ya kupoteza mahindi na maharagwe, mazao yenye thamani zaidi ya Sh50,000 mwaka wa 2009.

“Maeneo mengi Ukambani ni jangwa, na hushuhudia kiangazi na ukame. Nilipoteza mazao kufuatia majanga hayo,” asema, akikumbuka hasara aliyokadiria.

Ni hasara iliyomfumbua macho, akatathmini wazo jingine analotaja limegeuka kuwa la busara.

Zai pits, ni mfumo ambapo mashimo huandaliwa kwa makundi na kuwekwa mbolea asilia, ya mifugo ama samadi iliyochanganywa na majani na matawi ya mimea.

Vilevile, nyasi za boji (mulching) huwekwa kati ya mimea kuzuia uvukizi wa maji (evaporation).

Aidha, nyasi zinapaswa kuwa zilizokauka.

“Zilizokauka hazina wadudu wala magonjwa,” aelezea Timothy Mburu, mtaalamu na mkulima hodari wa mboga anayetumia nyasi za boji.

Urbanus huandaa mashimo yenye kipimo cha futi 2 kwa 2 na kina urefu wa futi mbili pia.

Kulingana na John Mutisya, mtaalamu kutoka Biovision Africa Trust, Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) lililoko Machakos na linalopiga jeki wakulima, mbali na muundo wa mraba, wa mviringo au nusu mviringo pia unaweza ukaandaliwa.

Mtaalamu John Mutisya kutoka Biovision Africa Trust, akieleza jinsi Zai pits zinavyotumika katika ukulima. PICHA | SAMMY WAWERU

Kwa mujibu wa maelezo ya mdau huyu, mahindi mashimo yanapaswa kupewa kipimo cha mita moja, mraba (1M square apart), akidokeza kwamba ekari moja inaweza kusitiri mashimo 400.

“Mbolea iliyoiva sambamba ichanganywe na udongo wa juu – uliotolewa kwenye shimo,” Mutisya ashauri.

Zai pit moja inapandwa hadi miche 5 ya mahindi.

Urbanus hutumia mfumo wa trei kukuza miche ya mahindi.

“Trei huniondolea kikwazo cha mbegu kuharibikia shambani mvua inapokosekana au kuchelewa,” asema mkulima huyo.

Mbali na kukumbatia mfumo wa Zai pits kukuza mahindi, pia huutumia kulima mboga na maharagwe.

Mifereji ya kunyunyizia mimea na mashamba maji, imesindikwa kandokando mwa mashimo.

Urbanus huvuna maji kupitia mabwawa, msimu wa mvua na kuyahifadhi kwenye matangi.

Zai pits hupunguza matumizi ya maji, wataalamu wakihimiza kukumbatiwa na wakulima wa jangwani na nusu-jangwa.

“Husaidia kudhibiti matumizi ya maji, kuyahifadhi muda mrefu na kuboresha rutuba ya udongo,” Mutisya asema.

Manufaa ya udongo hasa yanatokana na matumizi ya nyasi za boji, ambapo huboresha kiwango cha rutuba.

Kando na eneo tambarare, Zai pits pia hutumika katika kilimo cha mvungulio (green house).

Urbanus vilevile hukuza mahindi kwenye kivungulio.

Akihimiza wakulima kukumbatia mifumo ya teknolojia ya kisasa kuendeleza shughuli za kilimo, ndiyo Climate Smart Agriculture, hususan maeneo yanayoshuhudia uhaba wa mvua, mtaalamu Mutisya anasema huongeza kiwango cha mazao.

“Mabadiliko ya tabia nchi ni wazi na bayana, na hatuna budi ila kukumbatia mifumo ya teknolojia za kisasa kufanya kilimo, ili kukabili athari zake,” ashauri.

Athari za mabadiliko ya tabia nchi, haswa Barani Afrika zinaendelea kutatiza sekta ya kilimo na ufugaji, majanga ya ukame, magonjwa ya mimea na wadudu, yakizidi kuongezeka.

  • Tags

You can share this post!

Madaktari waahirisha mgomo baada ya kaunti kuahidi kuwalipa

Historia yawafaa Ruto, Raila 50:50

T L