• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Hofu huenda Hyundai isiwezane na barabara za Safari Rally

Hofu huenda Hyundai isiwezane na barabara za Safari Rally

Na GEOFFREY ANENE

Mashabiki wa magari ya Hyundai wameingiwa na wasiwasi kuwa magari hayo hayatafaulu Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally baada ya dereva Oliver Solberg kukumbwa na matatizo akifanya majaribio Juni 23 adhuhuri.

“Je, kuna uwezekano hata mdogo wa gari lolote la Hyundai kukamilisha mashindano haya? aliuliza seamus cassidy #104 (@bmw_racing) baada ya Oliver kuchapisha picha ya gari lake lililoharibika akitangaza kuwa gari lake limeharibika kidogo katika mkondo wa shakedown.

“Moja baada ya jingine, Safari Rally itatafuna timu ya Hyundai,” aliongeza Marc (@marceverymile).“Afadhali gari liliharibika katika majaribio ya shakedown kuliko katika mashindano yenyewe. Hata hivyo, najua kuna wale bado watakumbwa na matatizo hayo juma hili!” alisema Peter Taylor (@peter8171).

Baadaye Juni 23, Oliver Solberg alisema kuwa gari lake limerekebishwa na atakuwa mashindanoni yatakapoanza rasmi nje ya Jumba la KICC hapo Juni 24. “Tuko tayari kwa mashindano. Gari limerekebishwa na tumefanikiwa kufanya majaribio!” alisema Oliver.

Mbali na Oliver, madereva wengine watakaoendesha magari ya Hyundai katika Safari Rally inayorejea kwenye WRC baada ya miaka 19 ni bingwa wa 2009 Ott Tanak kutoka Estonia, Mbelgiji Thierry Neuville na Mhispania Dani Sordo.

Kampuni nyingine za magari ya WRC zinazowakilishwa katika mashindano hayo yatakayofanyika katika kaunti za Nairobi, Kiambu na Nakuru ni Toyota na Ford.Bingwa mara saba wa dunia Sebastien Ogier kutoka Ufaransa pamoja na Muingereza Elfyn Evans na raia wa Finland, Kalle Rovanpera wako katika timu ya Toyota nao Gus Greensmith (Uingereza) na Mfaransa Adrien Fourmaux wako katika timu ya Ford.

Wakenya watakaowania alama za WRC daraja ya tatu, Onkar Rai, Carl Tundo na Tejveer Rai wataendesha magari ya Volkswagen Polo GTI R5, Karan Patel (Ford Fiesta R5) naye Aakif Virani ana Skoda Fabia R5. Madereva wengi wa hapa nyumbani watapeleka magari ya Mitsubishi Lancer Evo X pia kuna magari ya Subaru Impreza.

  • Tags

You can share this post!

Droo ya Cecafa U23 kufanywa kupitia Zoom mnamo Ijumaa

Aina mpya ya virusi vya corona yaibua hofu India