• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Aina mpya ya virusi vya corona yaibua hofu India

Aina mpya ya virusi vya corona yaibua hofu India

AINA mpya ya virusi vya corona imevamia India huku serikali ikionya kuwa maafa makubwa huenda yakashuhudiwa tena nchini humo.

Wizara ya Afya jana ilisema kuwa watu 40 wamethibitishwa kuambukizwa aina mpya ya virusi vya corona vinavyojulikana kama Delta Plus (AY.1) katika majimbo ya Maharashtra, Kerala na Madhya Pradesh.

Taarifa ya serikali ilisema kuwa virusi vya Delta Plus vinasambaa kwa kasi na huenda vikasababisha maafa zaidi katika taifa hilo la Bara Asia.“Wataalamu wa Kukabiliana na Corona nchini India (INSACOG) wamegundua virusi vya Delta Plus katika majimbo matatu na kuna hatari ya kusambaa kote nchini,” ikasema taarifa ya wizara ya Afya.

Kamati ya INSACOG inajumuisha wataalamu kutoka Baraza la Kutafiti Matibabu nchini India na Taasisi ya Kutafiti Dawa Viwandani.Vipimo vilivyogundua virusi vya Delta Plus vilichukuliwa mwanzoni mwa Mei, mwaka huu.Watu milioni 30 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona nchini India na kati yao 390,600 wamefariki.

Visa zaidi ya milioni 16 na asilimia 50 ya vifo vilitokea ndani ya miezi minne iliyopita.Virusi vya corona, aina ya B.1.617.2, vilivyogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini India vilisababisha vifo vya maelfu ya watu ndani ya muda mfupi nchini India na kusababisha msongamano wa wagonjwa hospitalini.

Aina ya corona ya B.1.617.2, imegunduliwa katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Kenya (haswa ukanda wa Ziwa Victoria) na Uganda.Jana, wizara ya afya ya India ilisema kuwa aina mpya ya virusi vya corona (Delta Plus) ni hatari kwani vinaharibu mapafu na kushambulia kingamwili kwa kasi.Jana, India ilithibitisha visa vipya 50,848 vya maambukizi ya corona na vifo 1,358.

Wizara ya afya ilisema kuwa virusi vya Delta Plus tayari vimesambaa katika mataifa mengine 10, yakiwemo Uingereza, Amerika, Japan, Urusi, Ubeligiji, Uswisi, Nepal na China.Asilimia 20 ya maambukizi mapya ya corona nchini Amerika ndani ya wiki mbili zilizopita, yamesababishwa na virusi vya Delta Plus.

Visa 41 vya waathiriwa wa Delta Plus jana viliripotiwa nchini Uingereza. Jumla ya visa 200 vya watu walioambukizwa Delta Plus vimeripotiwa katika mataifa 11.Mtaalamu wa maradhi ya kuambukizwa nchini Amerika Anthony Fauci jana alisema kuwa angali anaamini kuwa chanjo za corona zinazotolewa zina uwezo wa kuzima makali ya Delta Plus.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa linafanya utafiti ili kubaini ikiwa chanjo zilizopo za kukabiliana na corona zinaweza kuzuia maambukizi ya virusi vya Delta Plus.

  • Tags

You can share this post!

Hofu huenda Hyundai isiwezane na barabara za Safari Rally

Bunge la Uganda lafungwa kwa wiki mbili kutokana na makali...