• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Hospitali ya Thika Level 5 yapokea dawa za Sh10 milioni

Hospitali ya Thika Level 5 yapokea dawa za Sh10 milioni

NA LAWRENCE ONGARO

HOSPITALI ya Thika Level 5 imepata afueni baada ya kupokea dawa za thamani ya Sh10 milioni.

Waziri wa Afya katika serikali ya Kaunti ya Kiambu Dkt Mbuthia Maina, amesema wamejitolea mhanga kuona ya kwamba hospitali zote zilizoko katika kaunti hiyo zinapata dawa za kutosha.

Leo Jumanne malori mawili yameleta dawa hizo katika Hospitali ya Thika Level 5 huku tahadhari ikitolewa kwa madaktari na wataalam wa dawa watumie dawa hizo kwa uwazi na kwa makini.

“Nimeshuhudia dawa zikipakuliwa kutoka kwa malori haya mawili. Nina imani zitanufaisha wagonjwa ambao hasa ndio walengwa,” amesema Dkt Maina.

Amesema yeye binafsi atafuatilia dawa hizo katika kila hospitali kuhakikisha zinasambazwa ipasavyo kwa wagonjwa wanaohitaji kupewa.

Hospitali ya Thika Level 5 imepokea dawa za Sh10 milioni. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Alisema kaunti hiyo pia itasambaza dawa kiasi cha thamani ya Sh63 milioni kwa hospitali nyingine katika gatuzi hilo.

“Wataalam watakaopatikana wakiuza dawa hizo wataachishwa kazi na baadaye kuchukuliwa hatua za kisheria,” alieleza Dkt Maina.

Alisema dawa zote zilizoletwa katika Hospitali hiyo ni za aina tofauti ambapo hakuna Daktari atatoa kisingizio kuwa hakuna dawa hospitali.

Baadhi ya dawa hizo ni za kutumika wakati wa kumfanyia mgonjwa upasuaji, ziko za kisukari, za damu kuchemka, na aina nyingine za kushughulikia maradhi kadha wa kadha.

Alitoa wito kwa wananchi kuwasiliana naye wakati wowote iwapo watashuku kuwa dawa hizo zinauzwa nje.

Alisema Gavana Kimani Wamatangi amefanya juhudi kuona ya kwamba sekta ya afya inaimarika kwa kasi.

Hapo awali wagonjwa wengi walipitia changamoto tele kwa sababu ya dawa kukosekana hospitalini.

Wagonjwa walikuwa wakilazimika kwenda nje kununua dawa.

“Tabia hiyo nitaizima kabisa ambapo mtu yeyote yule atakayeuza dawa hizo aandike chini kuwa siku zake zimewadia,” alionya Dkt Maina.

Alisema kila mgonjwa atakuwa na haki kupata matibabu bila kubaguliwa na daktari yeyote.

  • Tags

You can share this post!

Ruto na Mattarella wategua kitendawili cha mabwawa ya Arror...

Mwalimu akataa mimba aliyompa demu Valentino

T L