• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Renson Ingonga ateuliwa Mkurugenzi mpya wa Mashtaka ya Umma

Renson Ingonga ateuliwa Mkurugenzi mpya wa Mashtaka ya Umma

RICHARD MUNGUTI na CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amemteua Renson Ingonga kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).

Sasa jina la Ingonga litapelekwa kwa kamati ya Haki na Masuala ya Sheria ya Bunge (JLAC) kuchunguzwa na kupigwa msasa.

Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Tharaka George Gitonga Murugara.

Hadi kufikia uteuzi wake, Bw Ingonga alikuwa Naibu Mkurugenzi katika afisi ya DPP.

Dkt Ruto alimteua Ingonga kutoka kwa orodha ya watu 15 ambao walihojiwa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) kubaini ufaafu wao kwa wadhifa huo.

Aliwapiku wakili Danstan Omari, Thomas Letangule, David Ruto, Winston Ngaira, Peter Mailanyi, Jacob Ondari, James Ndegwa na David Okachi, Francis Andayi, Taib Ali, Jacinta Nyamosi, Victor Mule, Lilian Okumu, na Tabitha Ouya waliowania wadhifa huo.

Endapo JLAC itaidhinisha uteuzi wake na kamati ya bunge lote likubaliane na msimamo huo, Bw Ingonga atachukua nafasi iliyoachwa na Noordin Haji.

Bw Haji aliteuliwa na Rais Ruto kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa ya Ujasusi (NIS) mnamo Mei 2023.

Haji aliteuliwa DPP mnamo Agosti 2018 baada ya kuhudumu katika kitengo cha utafiti katika NIS.

Jopo la uteuzi wa DPP lilijumuisha watu saba wakiwemo Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU), Francis Atwoli na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak.

Wengine walikuwa Bi Mary Kimonye (Kutoka PSC) Shadrack Mose (Wakili Mkuu wa Serikali), Mary Adhiambo (Katibu Kitengo cha Masuala ya Wafanyakazi, Idara ya Utumishi wa Umma), Roseline Odede (Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu) na  Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Richard Obwocha.

  • Tags

You can share this post!

Sakaja aimarisha ukusanyaji mapato Nairobi

DK Kwenye Beat asema hapo kwa wash wash humpati

T L