• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Jinsi maafisa, viongozi walihusika katika sakata ya uuzaji wa ardhi ya shirika la reli South B

Jinsi maafisa, viongozi walihusika katika sakata ya uuzaji wa ardhi ya shirika la reli South B

Na SAMMY KIMATU

IMEFICHUKA kwamba maafisa wa utawala walishirikiana na wenyeviti wa mitaa ya mabanda ya Mukuru, South B katika sakata ya kuuza ardhi iliyomilikiwa na Shirika la Reli Nchini kuanzia mwaka 2000.

Hii ni baada ya tingatinga linalochimba ardhi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Aoko kuungana na barabara ya Entreprise kufunua mchanga na kupata reli.

Taifa Leo imebaini kwamba kwenye sakata hiyo, watu binafsi, makanisa na makundi ya miradi mbalimbali waliuziwa ardhi na kujenga nyumba juu ya reli.

Mdokezi wetu alisema baadhi ya maafisa wa utawala wa mikoa wakiwemo wakuu wa tarafa, machifu na wazee wa mitaa walihusika pakubwa kwenye ufisadi.

Baada ya kuuziwa eneo reli lililopitia, matapeli walimwaga tani nyingi za mchanga na kufunika reli kisha wakajenga nyumba za mabati na za mawe.

“Reli hii ilitumika hadi miaka ya tisini (1990s) ambapo gari la moshi lilileta bidhaa katika Taasisi ya Mafunzo ya Reli (RTI) kutoka kituo cha reli cha Makadara,” mdokezi akanena.

Juzi, tingatinga linalotumika katika ujenzi wa barabara katika mtaa wa Mukuru-Hazina lilichimba na kufikia mtambo wa reli na kusitisha shughuli siku hiyo.

‘’Hii ni aibu kubwa na inaonyesha jinsi maafisa wa serikali walivyojawa na tamaa. Ni lazima wakabiliwe kwa mujibu wa sheria ikiwa nchi itaenda mbele kimaendeleo,” mama mboga katika mtaa wa Hazina akanena.

Ili kudhihirisha uozo katika viongozi, katika eneo la kisa, duka moja linalouza vifaa vya muziki, nguo na viatu limesimama juu ya reli.

“Kuna kipande cha reli kilikatwa juu ya mto Ngong ili isionekane vile reli ilivyokuwa ikielekea kutoka upande wa Tetra Pak, barabara ya Likoni kuingia mtaa wa mabanda wa Hazina,” Ofisa wa polisi ambaye hatuwezi kumtaja kwa sababu tunajali usalama wake, akafichua.

Uchunguzi wetu pia ulibainisha kwamba kwa wale walionuia kujenga nyumba katika mtaa wa Hazina, waliuziwa ploti moja kuanzia Sh10,000.

“Ukiwa na Sh10,000 na umpelekee mzee wa mtaa pamoja na chifu, bila shaka unaonyeshwa ploti ya wewe kujenga nyumba ya vyumba vinne kwa hizo pesa,” mwanamume aliyehudumu katika ofisi ya KANU wakati huo akanena.

Aliongeza kwamba vijana katika ofisi za KANU enzi za utawala wa Rais Mstaafu Hayati Daniel Arap Moi walikuwa na nguvu nyingi na walikuwa wakiheshimiwa na kuogopwa mitaani.

“Kijana alikuwa na uwezo wa kukukamata na kukupeleka kituoni cha polisi na kukushtaki. Isitoshe, hungekarabati kibanda cha mboga kabla hujafahamisha ofisi ya KANU wakati huo,” Bw Cosmas Mutiso akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Kaunti zisipodhibitiwa nchi itaisha kwa...

Man-United wateua kocha Rangnick kushikilia mikoba yao hadi...

T L