• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Jirani wa shule asakwa akidaiwa kuweka sumu kwa chakula cha wanafunzi

Jirani wa shule asakwa akidaiwa kuweka sumu kwa chakula cha wanafunzi

NA OSCAR KAKAI

MAAFISA wa polisi katika mji wa Kapenguria wanamsaka mwanamume ambaye anadaiwa kuweka sumu kwenye chakula cha wanafunzi na walimu katika Shule ya Msingi ya Chepkoti, eneo la Siyoi, Kaunti ya Pokot Magharibi.

Mwanaume huyo anasemekana kuchanganya dawa ya panya na mafuta ya kupikia ya mpango wa msaada wa chakula shuleni kisha akaingia kwenye sanduku  moja na kuiba chumvi, maharagwe na Sh6,400 mnamo Alhamisi.

Haya yaligunduliwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo Bernard Chemiati baada ya kufungua ofisi hiyo na ghala la chakula ambalo liko karibu na ofisi yake na kupata vitu vimetawanyika.

Mwanamume huyo mshukiwa ambaye ni jirani wa shule hiyo ni mwanawe mzee ambaye aliuzia shule hiyo ardhi.

Kulingana na kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Pokot Magharibi Kipkemoi Kirui, mshukiwa huyo yuko mafichoni.

Bw Kirui alisema mshukiwa huyo huenda alikuwa na funguo ambazo alitumia kufungua ofisi na ghala ambalo lilikuwa na chakula.

“Tunashuku kuwa mwanaume huyo akiwa na wenzake wengine ambapo waliingia kwenye ofisi ya mwalimu mkuu Alhamisi usiku na kufanya maovu hayo. Mwalimu mkuu anasema kuwa alifunga mlango vyema na kupata uko sawa vile alifunga,” alisema.

Bw  Kirui alisema kuwa mafuta hayo ambayo yaliwekwa sumu yamepelekwa kwa maabara kuchunguzwa.

“Mwalimu mkuu aligundua kwa wakati baada ya kuona mafuta yamenyunyiziwa kemikali ambayo ni dawa ya panya. Chakula ambacho kilikuwa hapo kimepelekwa kupimwa kwenye maabara,” alisema.

Kulikuwa na hofu kwenye shule hiyo huku wazazi wakifika shuleni kujua hali ya kiafya ya watoto wao.

Masomo yaliathirika kutokana na hofu huku wazazi wakitaka familia ya mshukiwa kufurushwa.

Wakati huo huo, wazazi ambao walikuwa wamepiga kambi  kwenye uwanja wa shule walimtaka babake mshukiwa kuhama kutoka eneo hilo.

“Babake mshukiwa anasema kuwa anataka fedha zake Sh1 milioni ambazo ni masalio ya fedha za shamba kabla aondoke. Hata hivyo, babake haungi mkono kosa la mwanawe,” alisema Bw Kirui.

Bw  Kirui aliwataka wazazi kuwa na utulivu akisema uchunguzi unaendelea.

Mlinzi wa shule hiyo Bw Emanuel Kiplagat ambaye anasema kuwa hakuona yeyote akiingia kwenye shule, ameitwa kuhojiwa na polisi.

Mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Pokot Magharibi Simon Wamae alisema kuwa hakuna hatari sababu wanafunzi na walimu hawakuwa wamekula chakula chenyewe.

“Walishuku na kujua kwa wakati na hawakula chakula hicho. Tumewapatia chalula kingine kiwafae,” alisema Bw Wamae.

Bw Wamae aliwataka walimu wakuu kuwa chonjo kuhusu chakula cha wanafunzi na walimu shuleni.

  • Tags

You can share this post!

Tiba za nyumbani kwa kichefuchefu

Messi apachika wavuni bao la haraka zaidi kitaaluma na...

T L