• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Kafyu itaondolewa karibuni, asema Balala

Kafyu itaondolewa karibuni, asema Balala

Na MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Utalii, Bw Najib Balala amedokeza kuwa kafyu ambayo imedumu nchini tangu mwaka 2020 itaondolewa baada ya siku 30 zijazo.

Bw Balala alisema kwamba kafyu hiyo ambayo imeathiri uchumi na hasa sekta ya utalii, itaondelewa katika muda wa mwezi mmoja.

“Tuko na matumaini kwamba katika muda wa mwezi mmoja hivi, tutaweza kufungua,” Balala alisema katika kikao na wanahabari kwenye maonyesho ya Magical Kenya Travel Expo.

Kulingana na waziri, chanjo dhidi ya corona inayoendelea ni muhimu kwa kuwezesha nchi kufunguliwa na itainua imani ya watalii wa kimataifa kwa Kenya.

Kufungwa kwa nchi kama kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona kulifanya uchumi wa Kenya kudorora hadi asilimia -0.3 mwaka 2020 kutoka kiwango cha ukuaji cha asilimia tano mwaka wa 2019.

Balala alisema mazungumzo yanaendelea kati ya wizara husika kuondoa kafyu na kufungua uchumi wa nchi.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliongeza kafyu kwa siku 30 akisema kwamba japo maambukizi yamekuwa yakishuka, Kenya haijatimiza kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Shirika hilo linasema nchi huchukuliwa kuwa imedhibiti maambukizi ikirekodi chini ya asilimia tano kwa siku kumi na nne (14) mfululizo.

Balala alisema kwamba serikali inalenga kuchanja watu 10 milioni kufikia Desemba hatua ambayo itawezesha nchi kufunguliwa kikamilifu.

Mnamo Jumanne chama cha wafanyakazi wa mahoteli (KAHC) kiliomba serikali kuondoa kafyu.

You can share this post!

Watumishi wa Kaunti kugoma ‘wasipothaminiwa’

DOMO KAYA: Napenda kiki ya dizaini hii