• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
Kamishna Wanderi asema kuondolewa kwao hakutaisaidia IEBC na Kenya kufikia mageuzi katika mfumo wa uchaguzi

Kamishna Wanderi asema kuondolewa kwao hakutaisaidia IEBC na Kenya kufikia mageuzi katika mfumo wa uchaguzi

NA CHARLES WASONGA

KAMISHNA wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Francis Wanderi ndiye wa hivi punde kujiuzulu miongoni mwa makamishna wanne waasi ambao bunge lilipendekeza waondolewe afisini.

Kwenye barua ya kujiuzulu aliyoituma kwa Rais William Ruto, Bw Wanderi alitetea hatua yake na wenzake, ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati mnamo Agosti 15, 2022.

Makamishna wawili waliojiuzulu awali ni Justus Nyang’aya, ambaye alikuwa wa kwanza kujiondoa Ijumaa wiki jana, na Naibu Mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera aliyejiuzulu Jumatatu.

Lakini Kamishna Irene Masit ameshikilia kuwa hatajiuzulu huku wakili wake Donald Kipkorir akisema kuwa mteja wake yuko tayari kufika mbele ya jopo linaloongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule.

Makamishna hao wanne walipinga matokeo ya uchaguzi wa urais ambapo Rais Ruto alitangazwa mshindi wakida hakukuwa na uwazi katika hatua za mwisho za ujumuishaji kura.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Bw Wanderi ametetea hatua yake ya kupinga “matokeo yaliyotokana na udikteta, utovu na adabu na ukiukaji wa taratibu za kiutendakazi.”

“Nawasilisha barua yangu ya kujiuzulu leo (Alhamisi). Ninafanya hivyo si kwa sababu niko na hatia kutokana na madai niliyowekewa na wanaonishtaki lakini kwa sababu wakati umetimu ambapo masilahi ya taifa ni muhimu kuliko ya mwanadamu yakiwemo matumaini yangu ya kuwepo na mchakato wa kidemokrasia ya kusaidia nchini kufikia mageuzi katika masuala ya uchaguzi,” Bw Wanderi akasema kwenye barua yake.

Kamishna huyo alisema kujiuzulu kwake na wenzake, Cherera na Nyang’aya, au kupigwa kalamu kwao, “hakutaleta mabadiliko makubwa katika IEBC, wala kusaidia Kenya kufikia lengo lake la kuwepo na mageuzi katika mfumo wa uchaguzi nchini.”

You can share this post!

Bazara la Mawaziri launga azma ya Kenya kuandaa AFCON 2027

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Jinsi Morocco walivyotoa miamba...

T L