• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 12:38 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Jinsi Morocco walivyotoa miamba Uhispania pumzi

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Jinsi Morocco walivyotoa miamba Uhispania pumzi

Na MASHIRIKA

ACHRAF Hakimi alifungia Morocco penalti ya ushindi na kusaidia mabingwa hao wa Afrika 1976 kudengua Uhispania kwa mikwaju 3-0 baada ya pambano lao la hatua ya 16-bora kukamilika kwa sare tasa chini ya dakika 120 uwanjani Education City.

Ni mara ya pili mfululizo kwa Uhispania kuondolewa katika hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia kwa mikwaju ya penalti baada ya Urusi kuwadengua kwa mikwaju 4-3 baada ya sare ya 1-1 katika raundi hiyo mnamo 2018.

Kipa Yassine Bounou wa Morocco alipangua penalti mbili kutoka kwa Carlos Soler na Sergio Busquets na kuhakikisha kuwa timu yake ya taifa inatinga robo-fainali kwa mara ya kwanza katika historia.

Mkwaju uliochanjwa na Pablo Sarabia uligonga mhimili wa goli la Morocco ambao sasa watakutana na Ureno walioponda Uswisi 6-1 katika pambano jingine la raundi ya 16-bora.

Morocco sasa ni kikosi cha nne kutoka Afrika baada ya Cameroon (1990), Senegal (2002) na Ghana (2010) kuwahi kutinga robo-fainali za Kombe la Dunia.

Hadi kufikia mwaka huu wa 2022, Morocco waliwahi kuingia hatua ya 16-bora kwenye Kombe la Dunia mnamo 1986. Sasa wameweka rekodi ya kutoshindwa katika mechi tano za Kombe la Dunia na kutofungwa katika michuano sita kati ya saba katika mashindano yote. Morocco hawajashindwa katika Kombe la Dunia tangu waambulie sare ya 2-2 dhidi ya Uhispania mnamo Juni 2018 nchini Urusi.

Kudenguliwa kwa Tunisia, Ghana na Cameroon katika hatua ya makundi; na kuondolewa kwa Senegal katika raundi ya 16-bora kwenye makala ya mwaka huu, kumeacha matumaini ya Afrika mikononi mwa Morocco.

Masogora hao wa kocha Walid Regragui walitamalaki Kundi F kwa alama saba, mbili kuliko Croatia waliopigwa 4-2 na Ufaransa katika fainali ya Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi. Walianza kampeni za kundi lao kwa sare tasa dhidi ya Croatia kabla ya kuduwaza miamba Ubelgiji 2-0 na kupepeta Canada 2-1.

Uhispania waliotawazwa wafalme wa dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini, walifungua kampeni za makundi mwaka huu kwa ushindi mnono wa 7-0 dhidi ya Costa Rica. Walipokea kichapo cha 2-1 kutoka kwa Japan katika pambano la mwisho baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Ujerumani – mabingwa mara nne wa dunia ambao pia waliokota pointi nne.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kamishna Wanderi asema kuondolewa kwao hakutaisaidia IEBC...

USHAURI NASAHA: Thamini mazoezi ya kimwili hata sasa...

T L