• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Kampuni ya maji yajengea shule darasa la kisasa

Kampuni ya maji yajengea shule darasa la kisasa

NA LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya maji ya Thika (THIWASCO) imejitolea kujenga darasa moja katika Shule ya Msingi ya Gatuanyaga, Thika Magharibi.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Bw Moses Kinya, amesema lengo lao kuu ni kuijali jamii kwa kutoa misaada.

“Tumejitolea kujenga darasa moja litakalopunguza msongamano uliopo katika shule hiyo,” alisema Bw Kinya.

Shule ya Gatuanyaga ina idadi ya wanafunzi wapatao 1,500 na tatizo la uhaba wa madarasa ya kutosha si geni.

Kuhusu ukosefu wa maji, mkurugenzi huyo alisema ukame ulioshuhudiwa majuzi umlisababisha mito ya Chania na Thika kukauka na kusababisha kampuni hiyo kupunguza kiwango cha maji inayosambaza katika mji wa Thika.

Hata hivyo alisema bado wana ushirikiano na shirika la kimataifa la Denmark – DANIDA – katika maendeleo yanayohusu usambazaji wa maji.

“Tunatoa wito kwa wakazi wa Thika kwa jumla kutumia maji kwa uangalifu bila kunyunyizia kwenye mashamba na uoshaji wa magari,” alisema Bw Kinya.

Hata hivyo alisema kampuni imejitolea kuweka vituo kadha vya maji mijini vitakavyotumiwa na wananchi wanapotaka kukata kiu yao.

“Tunaelewa vyema utumizi wa maji na wananchi upo juu sana na kwa hivyo kampuni inajaribu kwa njia zote kuwapa maji,” akasema.

Mwenyekiti wa kampuni ya THIWASCO, Bw Joseph Kimani amesema kampuni hiyo itafanya juhudi hata kuzisaidia shule kadha kwa vifaa muhimu kama matangi ya kuhifadhi maji kwa lengo la kuziba shida ya maji inayoshuhudiwa kila sehemu eneo la Thika na vitongoji vyake.

Kulingana na mwenyekiti huyo, darasa lililojengwa katika shule ya Gatuanyaga liligharimu takribani Sh1.5 milioni.

Walimu katika shule hiyo walipongeza kampuni hiyo kwa kazi nzuri.

  • Tags

You can share this post!

Unga: Chapa zinazopendwa zingali ghali

Tuchel akiri matatizo yaizonga Bayern Munich

T L