• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Harry Kane aongoza Spurs kupepeta Crystal Palace katika gozi la EPL

Harry Kane aongoza Spurs kupepeta Crystal Palace katika gozi la EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Antonio Conte wa Tottenham Hotspur amesema itakuwa “vigumu sana” kutomchezesha Harry Kane katika baadhi ya mechi za kikosi hicho msimu huu.

Hii ni baada ya fowadi huyo raia wa Uingereza kufunga bao lake la pili baada ya ukame wa muda mrefu wa magoli katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kuongoza Spurs kutandika Crystal Palace 3-0 mnamo Jumapili.

Kane alifungulia waajiri wake ukurasa wa mabao katika dakika ya 32 kabla ya mengine kufumwa wavuni kupitia kwa Lucas Moura na Son Heung-min kunako dakika za 34 na 74 mtawalia.

Kane ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza, alikuwa amepachika wavuni bao moja pekee ligini kabla ya Disemba 19, 2021. Hata hivyo, magoli dhidi ya Liverpool na Palace sasa yamemridhisha zaidi Conte.

“Kane ni miongoni mwa wavamizi bora zaidi duniani na ni mchezaji ambaye ana umuhimu mkubwa kambini mwa Spurs,” akatanguliza Conte.

“Leo nilipata fursa ya kupumzisha kidogo baada ya kumchezesha kwa dakika 60 pekee. Lakini naona ugumu wa kutomwajibisha katika mechi yoyote ijayo. Amefunga bao ambalo naamini litamwamshia hamu ya kutaka kutaka mengine zaidi,” akaongeza mkufunzi huyo wa zamani wa Chelsea, Juventus na Inter Milan.

Conte alimuondoa Kane uwanjani baada ya dakika 60 ili kumpa nafasi mwafaka ya kujiandaa vilivyo kwa mechi dhidi ya Southampton na Watford watakaovaana nao chini ya siku sita zijazo.

Spurs hawajawahi kushindwa katika mechi sita ligini chini ya Conte na kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama 29, sita nyuma ya Arsenal wanaofunga orodha ya nne-bora. Hata hivyo, Spurs wana mechi tatu zaidi za kutandaza ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na Arsenal waliokomoa Norwich City 5-0 mnamo Jumapili.

Palace walikuwa wameomba wasimamizi wa EPL kuahirisha mechi hiyo iliyowakutanisha na Spurs kwa sababu ya maambukizi corona ambayo pia yamempata kocha wao Patrick Vieira.

Kutokuwepo kwa Vieira ambaye kwa sasa anajitenga, kulisaza Palace katika ulazima wa kutegemea maarifa ya kocha msaidizi Osian Roberts kusimamia kikosi kilichocheza kwa takriban dakika 60 bila mchezaji mmoja.

Hii ni baada ya fowadi matata Wilfried Zaha kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano na kufurushwa uwanjani katika dakika ya 37. Palace almaarufu ‘The Eagles’ sasa wanashikilia nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 20 sawa na Brentford na Southampton waliopepeta West Ham United 3-2 uwanjani London Stadium.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kanisa lakosoa chanjo ya lazima

Arsenal waponda Norwich City na kumtia kocha Dean Smith...

T L