• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kaunti yakarabati barabara mbovu ingawa maarufu

Kaunti yakarabati barabara mbovu ingawa maarufu

Na RUTH MBULA

SERIKALI ya Narok imeanza kukarabati barabara mbovu ya Murkan-Sosiana, miezi mitatu baada ya mkuu wa Shule ya Sosiana kuangaziwa akitembea matopeni umbali mrefu kwenda kuchukua karatasi za Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE).

Serikali ya Kaunti imeanza kukarabati barabara ya Juction-Bogoria inayoelekea katika lango kuu la shule hiyo.

Walimu, wahudumu wa bodaboda na wenye magari sasa wanaitumia bila hofu ya kushambuliwa na wahalifu.

Bi Magdalene Kimani alikuwa akitembea umbali wa kilomita 10 kwenda kuchukua karatasi za mtihani kwa ajili ya watahiniwa 18 wa shule yake iliyoko Trans Mara Mashariki, Kaunti ya Narok.

Taifa Leo ilitembelea mradi huo Jumanne na kubaini kuwa ukarabati unaendelea.

Mitaro ya kupitisha maji ya mvua inaponyesha pia imeanza kujengwa.

Inakadiriwa kwamba Bi Kimani alitembea jumla ya umbali wa kilomita 320 tangu mtihani wa KCSE ulipoanza na kumalizika. Umbali huo ni sawa na kutembea kutoka Nairobi hadi mjini Bungoma.

Bi Kimani ni mfano tu wa watu ambao wamekumbwa na masaibu ambayo walimu katika maeneo ya vijijini hupitia wakati wa mtihani.

Bi Kimani alirauka alfajiri na kupitia barabara yenye tope ya Murkan-Sosiana iliyozungukwa na vichaka na kisha kuvuka mto Kibailuk.

Habari kuhusu masaibu ya mwalimu huyo iliwakera baadhi ya maafisa katika wizara ya Elimu ambao walimtaka kuandikisha taarifa.

Vyama vya walimu vilishutumu vikali agizo hilo la wizara ya Elimu.

Lakini baadaye, Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ilisema kuwa haina lengo la kumwadhibu Bi Kimani na badala yake itamtunuku kutokana na juhudi zake.

Mkurugenzi Mkuu wa TSC, Nancy Macharia alisema kuwa mwalimu huyo atatunukiwa pamoja na walimu wengine ambao wametia fora katika majukumu yao.

Kufikia sasa Bi Kimani hajatuzwa na TSC huku wakazi wa eneo la Trans Mara wakisema kuwa mwalimu huyo ni shujaa wao.

“Tunamshukuru sana Bi Kimani kwani juhudi zake zimefanya serikali ya kaunti hii kukarabati barabara hii ambayo imekuwa mbovu kwa muda mrefu,” akasema Bw Amos Cheruiyot, mkazi.

Bi Grace Chemutai alisema kuwa sasa wanatumia bodaboda kwenda na kutoka Sosiana –jambo ambalo halikuwezekana miezi mitatu iliyopita.

“Tunaomba kwamba mradi huo ukamilishwe na barabara ijengwe kwa kiwango cha lami,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Kitita cha Sh.6Milioni kilipatikana katika afisi za majaji...

Kenya Lionesses wazidiwa maarifa na New Zealand raga ya...