• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
KCPE: Kaunti za Kwale na Kilifi zawika Pwani

KCPE: Kaunti za Kwale na Kilifi zawika Pwani

NA WAANDISHI WETU

KAUNTI za Kwale na Kilifi zilitamba ukanda wa Pwani katika matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) yaliyotangazwa Jumatano.

Takwimu zilizokusanywa kwa njia huru na Taifa Leo, zilionyesha idadi kubwa ya watahiniwa waliozoa alama zaidi ya 400 walitoka katika shule zilizoko kaunti za Kwale na Kilifi, wakifuatwa na Mombasa.

Shule nyingi kati ya hizo zilizotia fora zilikuwa ni za kibinafsi.

Kwenye orodha hiyo, mwanafunzi aliyeibuka nafasi ya kwanza Pwani kufikia wakati wa gazeti kuchapishwa, alikuwa ni Ngigi John Kariuki, kutoka shule ya msingi ya Bambino iliyoko Kilifi. Alijizolea jumla ya alama 427.

Bi Jane Wanjue, ambaye ni mamake Ngigi, alisema mwanawe amekuwa akipata matokeo bora shuleni tangu alipoanza chekechea. Alijiunga na shule ya Bambino Academy katika darasa la nne, na akawa akiongoza kwenye mitihani kila wakati.

“Kariuki alikuwa katika nafasi tatu bora kila mara walipofanya mitihani. Sikutarajia angefanya vyema kiasi hiki lakini nimefurahi kwa vile ametuletea fahari kuu,” akasema Bi Wanjue.

Wakati mwingi, mvulana huyo hupenda kuchora na kusoma badala ya kucheza nje.

Hata hivyo, hajaamua kuhusu mipango yake ya miaka ya usoni.

“Ninachoamini ni kuwa ataendelea kufana katika chochote kile atakachoamua kufanya miaka ijayo,” akasema mamake.

Baadhi ya shule za umma za Pwani zilizotoa watahiniwa bora ni Ganjoni iliyoko Mombasa na Lake Kenyatta kutoka Lamu.

Aisha Athman Mohamed wa Ganjoni alipata alama 417 huku Ngaruiya Peter Mburu wa Lake Kenyatta iliyoko Mpeketoni akipata alama 413.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Mburu alimshukuru Mungu kwa kumwezesha kufanya vyema. Alisema azma yake ni kuwa daktari wa upasuaji.

“Bidii zangu na nidhamu ndizo zimeniwezesha kufanya vyema na nimefurahi,” akasema Bw Mburu.

Kwa mara nyingine, shule ya msingi ya Masimbani, ambayo ni ya umma katika eneo la Kwale, ilipata matokeo bora ambapo mwanafunzi wa kwanza alizoa alama 412, huku wengi wakiwa na alama zaidi ya 400.

Orodha ya awali ya matokeo ilionyesha kulikuwa na ushindani wa hapa kwa hapa kati ya watahiniwa wa kike na kiume ukanda wa Pwani.

Ripoti za Brian Ocharo, Kalume Kazungu na Siago Cece

You can share this post!

KCPE 2022: Fadhili Nathan Chara wa Little Angels aibuka wa...

Benzema aangika daluga za gozi la timu yake ya taifa

T L