• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kenya kusafirisha shehena kubwa zaidi ya mbegu ya ng’ombe wa kiasili

Kenya kusafirisha shehena kubwa zaidi ya mbegu ya ng’ombe wa kiasili

Na JAMES MURIMI

Kenya itafikia hatua muhimu hivi punde kwa kusafirisha idadi kubwa ya mbegu za ng’ombe aina ya Borana na Ankole kwa taifa la nje.

Kikosi cha wanasayansi kimekamilisha mradi wa kuandaa viinitete (embryo) 2,954 katika kituo cha Sirima, kwenye hifadhi ya Ol Pajeta, Kaunti ya Laikipia tayari kusafirishwa Afrika Kusini.

Aina hizo za ng’ombe ambazo ni viinitete 1,353 vya Boran na 1,601 vya Ankole zinasakwa mno katika sehemu nyingi barani Afrika na usafirishaji wake utaunda uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili.

Kituo hicho cha Sirima kimekuwa kikifanya majaribio ya kibayoteknolojia kwa zaidi ya miaka 20 kwa ushirikiano na shirika la Afrika Kusini linaloitwa Embryo Plus.

Meneja Mkurugenzi wa shirika hilo Dkt Morne De La Rey anasema kwamba mradi huo ni hatua muhimu ambayo itahakikisha kwamba hakuna usambazaji maradhi ya ng’ombe kutoka kwa ng’ombe, hatua itakayohakikisha kwamba ndama walio na afya nzuri wanazaliwa Afrika Kusini.

“Hii itakuwa shehena kubwa zaidi ya viinitete kuwahi kusafirishwa baina ya nchi mbili kote duniani. Ni mradi muhimu ambao utaimarisha uhusiano baina ya Kenya na Afrika Kusini. Ni moja ya mkataba mkubwa zaidi wa kibiashara ambao umesainiwa baina ya mataifa haya mawili,” akasema Dkt Morne.

Wataalamu hao, kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Laikipia wametia saini mkataba kabla ya kufunga chupa zilizo na viinitete hivyo tayari kusafirishwa kwenda Afrika Kusini ambako kutafanyika katika wiki mbili zijazo.

Hifadhi hiyo ya hekari 90,000 ina ng’ombe 6,000 wa Boran ambao huchaguliwa kwa makini kwa ajili ya kuvuna viinitete.

Meneja wa kituo hicho, Bw Eugene Gachii anasema wao hukusanya sampuli kutoka kwa wanyama hao na kuwapima maradhi kadhaa ili kuhakikisha kwamba fahali wako na afya nzuri kabla ya kuanza hatua za kuvuna viinitete.

Kituo hicho katika miaka ya hivi karibuni kimeibuka kuwa kikubwa zaidi katika usafirishaji wa viinitete wa Boran ambao wanafahamika kwa uvumilivu mkubwa wa hali ya anga.

Afrika Kusini iliagiza viinitete vya Boran vya kwanza kutoka kwa hifadhi hiyo ya Ol Pajeta mnamo 1994 na idadi hiyo imekua hadi sasa imefikia 40,000.

  • Tags

You can share this post!

Tanzania yaambia raia waweke akiba nzuri ya mchele na...

Silambi matapishi, Pique amjibu Shakira zogo la mapenzi...

T L