• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Silambi matapishi, Pique amjibu Shakira zogo la mapenzi likiendelea

Silambi matapishi, Pique amjibu Shakira zogo la mapenzi likiendelea

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

MWANASOKA mstaafu raia wa Uhispania, Gerard Pique, 36, ametaka sasa aliyekuwa mkewe, Shakira Isabel, kumkoma kabisa huku akiapa kwamba “hakuna chochote kinachoweza kumfanya arudiane naye kimapenzi.”

Sogora huyo wa zamani alivunja kimya wiki hii, siku chache baada ya Shakira kuachilia kibao kipya ‘The Boss’, alichotumia kumsuta Pique kwa vijembe tele.

Kabla kuangushia mashabiki wimbo huo mpya katika hafla ya kutolewa kwa tuzo za MTV Video Music jimbo la New Jersey, Amerika, Shakira alighani mistari michache ya kibao chake cha awali.

“Thamani yangu ni zaidi ya maradufu ya wasichana wawili wenye umri mdogo wa miaka 22. Mimi ni Ferrari, si gari dogo kama Twingo. Tangu lini saa ya Rolex ikalinganishwa na Casio?”

Sawa na kibao chake cha awali, wimbo mpya wa Shakira, 46, bado unamchamba Pique aliyetemana naye Juni 2022 baada ya kuwa pamoja katika ndoa kwa miaka 11.

Isitoshe, unamdunisha sana kisura Clara Chia Marti – mchumba mpya wa Pique aliyesambaratisha penzi la sogora huyo wa zamani wa Barcelona na Shakira.

“Huenda bado hajashiba umaarufu. Ila ningeomba akome jina langu katika nyimbo zake maadamu sijishughulishi na maisha yake,” akasema Pique katika mahojiano na gazeti la The Sun.

“Asonge mbele na maisha bila kunifanya ajenda ya ngoma zake,” akaongeza na kufichua ‘The Boss’ ni jina ambalo marafiki wake wa karibu, hasa wanasoka, walimpa Shakira kwa sababu ya “ukali na majivuno”.

“Shakira asingetaka hata nialike marafiki zangu wa kiume nyumbani. Hata ningefanya hivyo kwa lazima, angewalaki kwa moyo baridi,” akasema Pique ambaye kwa pamoja na Shakira wana watoto wawili – Milan na Sasha.

Huku uhusiano wa Pique na Clara ukinoga hadi kufikia sasa wanapopanga kula yamini ya ndoa, Shakira tayari ametemana na dume lake jipya, Lewis Hamilton, 38, ambaye ni dereva maarufu wa magari ya Langalanga.

Mnamo Julai, Shakira aliungama kuwa “anakaribia kupata hifadhi mpya ya penzi lake kwa Hamilton” baada ya kuanza kuonekana mara kwa mara na dereva huyo wakiponda raha na kuhudhuria hafla nyingi pamoja.

Hata hivyo, inakisiwa kuwa wawili hao wametofuatiana kuhusu mpango wa kuanza familia na kupata watoto pamoja.

“Hamilton ana haja ya kutulia katika ndoa na kupata watoto. Shakira hataki kabisa uhusiano wa sampuli hiyo. Hana mpango wa kuwa mjamzito,” akasema mnajimu raia wa Jamhuri ya Domican, Nino Prodigio, ambaye ni rafiki na msiri wa Hamilton.

  • Tags

You can share this post!

Kenya kusafirisha shehena kubwa zaidi ya mbegu ya ng’ombe...

Hunter amweka babake Rais Biden wa Amerika pabaya kwa...

T L